Meneja wa
Huduma za Maabara ya Tume ya Madini, Mhandisi Mwarabu Mvunilwa amewaalika wadau
wa sekta ya madini nchini kutumia maabara ya kisasa ya Tume kwa huduma za
uhakika na viwango vya kimataifa.
Akizungumza
kupitia mahojiano maalum amesema kuwa maabara hiyo, ipo katika Jengo la TIRDO
Complex, Msasani – Dar es Salaam, na imekuwa ikihudumia wachimbaji,
wafanyabiashara wa madini, wawekezaji pamoja na taasisi mbalimbali kwa huduma
za uchambuzi na ushauri wa kitaalamu.
Mhandisi
Mvunilwa amesema kuwa maabara hiyo ya serikali imewekewa teknolojia ya kisasa
ikiwemo mashine za X-Ray Fluorescence (XRF) na fire assay furnaces zinazotoa
matokeo ya haraka, sahihi na yenye gharama nafuu.
“Tunatoa huduma zinazokidhi viwango vya
kimataifa vya ISO 17025. Matokeo yetu yanakubalika ndani na nje ya nchi, hivyo
kuwa msingi wa uwazi katika biashara ya madini,” amesema.
Huduma
zinazotolewa na maabara hiyo ni pamoja na uchambuzi wa madini ya metali kwa kutumia XRF, vipimo vya dhahabu na
fedha kwa njia ya fire assay, acid digestion + AAS kwa metali za msingi,
uhakiki kiasi cha dhahabu na utambuzi wa madini, pamoja na upimaji na
maandalizi ya sampuli. Huduma nyingine ni vipimo vya unyevu na loss on ignition
vinavyowezesha wachimbaji kupata taarifa sahihi za kijiolojia.
Kwa
mujibu wa Mhandisi Mvunilwa, maabara hiyo inaendeshwa na wataalamu waliobobea
katika nyanja za jiokemia, madini na metallojia ambao hutoa matokeo yenye
uhakika kwa ajili ya kusaidia maamuzi ya kiuchumi na kiuwekezaji.
Ameongeza
kuwa huduma hizo zimekuwa chachu ya kuongeza thamani ya madini na mapato ya
serikali kupitia usahihi na uaminifu wa taarifa zinazotolewa.
Amesisitiza
kuwa huduma za maabara hiyo si za ndani pekee bali pia zinatambulika kimataifa
na hutumiwa na wateja kutoka mataifa mbalimbali, jambo linaloimarisha nafasi ya
Tanzania katika biashara ya madini duniani.
Wadau wa
sekta ya madini wanahimizwa kutembelea maabara hiyo iliyopo TIRDO Complex,
Msasani – Dar es Salaam au kuwasiliana kupitia barua pepe
lab.coordinator@tumemadini.go.tz, simu 0733 010 338 au kupitia tovuti rasmi ya
Tume ya Madini www.miningcommission.go.tz/laboratory
0 Maoni