WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Waandishi wa
Habari nchini kutumia Akili Mnemba (Artificial Inteligence) kama nyenzo ya
kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo na sio kikwazo cha uhuru wao.
Amesema kuwa katika dunia ya sasa, vyombo vya habari
vinakutana na changamoto mpya zinazotokana na maendeleo ya teknolojia, ambapo
akili mnemba inachukua nafasi kubwa katika uzalishaji na usambazaji wa habari.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Aprili 29, 2025)
katika Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, ambayo
kitaifa inafanyika Jijini Arusha kwenye Hoteli ya Gran Melia.
Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kuandaa sera maalum
ya Akili Mnemba, ambayo itatoa mwongozo wa matumizi yake katika vyombo vya
habari ili kuhakikisha kuwa teknolojia hiyo inaendana na misingi ya uhuru wa
vyombo vya habari, uwazi, na uadilifu wa uandishi wa habari.
“Ni ukweli usiopingika kwamba, Akili Mnemba inaweza kuwa
msaada mkubwa kwa wanahabari, lakini pia inaweza kuwa chanzo cha changamoto
kubwa ikiwa haitatumika kwa busara. Hili linahitaji mjadala wa wazi, sera
madhubuti, na ushirikiano wa karibu kati ya sekta zote.”
Amesema Serikali ya Tanzania inatambua na kuthamini mchango
mkubwa wa vyombo vya habari katika maendeleo ya Taifa, kwa kupitia vyombo vya
habari, imeweza kuwahabarisha wananchi kuhusu shughuli na mipango ya Serikali,
kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za kimaendeleo.
Amesema viongozi wanatambua na kuthamini mchango mkubwa wa
waandishi wa habari na vyombo vya habari katika kuhabarisha jamii, kuhimiza
uwajibikaji na kuimarisha demokrasia nchini. Aidha, wanawahimiza kuendelea
kufanya kazi kwa weledi, maadili na uzalendo kwa ajili ya mustakabali wa
wananchi na dunia kwa ujumla.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema vyombo vya habari
vimekuwa sehemu muhimu katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala
mbalimbali, ikiwa ni pamoja na elimu ya uzalishaji, ujasiriamali, na maendeleo
ya kijamii.
Waziri Mkuu ameongeza kwa kusema kuwa vyombo vya habari
vimekuwa na nafasi kubwa katika kulinda na kudumisha amani, umoja, na
mshikamano wa kitaifa na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuijenga taswira
chanya ya Tanzania kimataifa.
Naye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa
Palamagamba Kabudi amesema kuwa Akili Mnemba isiwafanye waandishi wa habari
nchini wakafubaa na badala yake wahakikishe wanaitumia vizuri katika
utekelezaji wa majukumu yao.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Gerson Msigwa ametumia fursa hiyo kuwapongeza waandishi wa habari kwa
kuendelea kupambania matumaini ya wananchi.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa mwaka 2025 inasema: “Uhabarishaji kwenye Dunia Mpya: Mchango wa Akili Mnemba (AI) katika Uhuru wa Vyombo vya Habari.”
0 Maoni