Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi amefungua mafunzo ya siku tatu kuhusu
elimu ya utalii wa anga (astrotourism) yaliyoanza leo tarehe 19 Septemba, 2025
Karatu Mkoani Arusha.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na
Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu
Huria cha Tanzania (OUT) yanatolewa na wataalamu wabobezi kutoka taasisi za
Astrotourism Aotearoa (AAA) kutoka nchini New Zealand, Smithsonian
Astrophysical Observatory (SAO) ya Chuo Kikuu cha Harvard pamoja na taasisi ya kimataifa ya Dark Sky
International yenye Makao Makuu Jijini Arizona, Marekani.
Akifungua mafunzo hayo Dkt. Abbas
amesema utoaji wa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Wizara ya Maliasili na
utalii kufungua mazao mapya utalii ikiwepo utalii wa Anga ambapo hatua ya sasa
ni kutoa mafunzo, maarifa na ujuzi kwa watanzania kuhusu utalii wa anga, vifaa
vinavyotumika na fursa zilizopo katika aina hiyo ya utalii.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu
huria cha Tanzania Prof. Saganga Kapaya ameeleza kuwa Tanzania inazo fursa
nyingi za utalii wa anga, ambao ni bidhaa mpya ya utalii hapa nchini kwa kuwa
zaidi ya theluthi moja ya ardhi ya Tanzania imehifadhiwa, na hivyo kupelekea
maeneo yake mengi kuwa na anga lenye giza wakati wa usiku hivyo kuwezesha anga kuonekana kwa zaidi ya asilimia 95
ukilinganisha na mataifa mengine Afrika.
Prof. John Hearnshaw kutoka New
Zeland ambaye ni mwezeshaji wa mafunzo hayo ameeleza kuwa mafunzo yatajikita
katika maeneo manne ambayo ni namna ya kuendesha utalii wa anga kwa
kushirikisha wadau wa utalii na Jamii, utalii wa anga na Fizikia anga, matumizi
ya Telescopic pamoja na upigaji wa picha za utalii wa anga.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na
washiriki zaidi ya 70, ambao ni wasafirishaji watalii (Tour Operators),
waongoza watalii (tour guides), waendeshaji wa huduma za malazi (Hoteliers ),
taasisi za serikali zinazohusika na kutangaza utalii (TTB na ZCT), taasisi za
uhifadhi (NCAA, TANAPA, TAWA, na TFS), taasisi za elimu, mafunzo na utafiti
(NCT, ACWM-Mweka, VETA, na OUT), Wataalamu wa Utalii, Wasimamizi wa Utalii,
Watafiti, Waandaaji wa sera na wafanya maamuzi, Wana-astronomia, Wanafunzi,
Wajasiriamali, na watunga sera.
Na. Kassim Nyaki - Karatu
0 Maoni