Mgombea Ubunge wa Jimbo la
Bukombe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Doto Mashaka Biteko amewaasa
wananchi kushiriki katika zoezi la upigaji kura Oktoba 29 ili kuchagua viongozi
watakaoweza kutimiza matarajio yao ya kuwaletea maendeleo.
Dkt. Biteko amesema hayo Septemba
19, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Lyambamgongo wilayani
Bukombe mkoani Geita ikiwa ni sehemu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge
na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
“ Uchaguzi ni uwekezaji wa
maisha, kupiga kura na kuchagua viongozi inakupa uhalali wa kudai maendeleo
kutoka kwa wale uliowachagua. Mimi huwa nashangaa mtu hapigi kura wala
haudhurii vikao vya maendeleo lakini anakuwa wa kwanza kulalamika,” amesema
Dkt. Biteko.
Amesema wapiga kura wa Kata hiyo
4,600 waliojiandikisha wajitokeze kupiga kura na kuichagua CCM ili katika
kipindi cha miaka mitano ijayo iwaletee maendeleo.
Ametaja baadhi ya mikakati ya CCM
katika Kata hiyo kuwa ni kuwaletea gari ya wagonjwa pamoja na kufikisha umeme
katika vitongoji saba ambavyo havijafikiwa na umeme.
Fauka ya hayo, amewaeleza
wananchi hao kuwa katika uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwaruhusu
wananchi wa Bukombe kuchimba madini katika Pori la Kigosi ili wapate fursa ya
kujipatia kipato.
Pia, amesema Wilaya ya Bukombe
haikuwa na stendi, soko la kisasa wala jengo la halmashauri hata hivyo Dkt.
Samia ametoa fedha kwa ajili wa utekelezaji wa miradi hiyo hivyo wamchague kwa
kumpa kura nyingi Oktoba 29.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko
amewaasa wananchi kutogawanyika kwa sababu yoyote ile hususan wakati wa
Uchaguzi Mkuu.
Naye, Mgombea wa Udiwani Kata ya
Lyambamgongo, Boniface Shitobero amemshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa
fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara, zahanati mbili, madarasa na vifaa
vya maabara katika shule za sekondari.
“ Kuna shule shikizi ambayo
ametuletea fedha kwa ajili ya kujenga madarasa, kila kijiji kina umeme,”
amesema Shitobero.
Aidha, amesema CCM ikipewa ridhaa
ya kuongoza kwa miaka mitano ijayo itatekeleza miradi mipya kama shule na
hospitali.
0 Maoni