Sekta ya
Madini nchini inaendelea kushuhudia mageuzi ya kuongeza thamani madini yakiwemo
ya ujenzi kama mchanga na kufungua fursa nyingine mpya kwa wachimbaji wadogo wa
mchanga kupitia teknolojia bunifu za usindikaji.
Katika
mkoa wa Tanga, Kampuni ya Muwa Trading Tanzania Limited imewekeza kwenye
Kiwanda cha kuosha na kusafisha mchanga kwa maji ili kuondoa udongo na uchafu
mwingine kama mizizi, hatua ambayo imebadilisha kabisa mtazamo wa thamani ya
rasilimali hiyo kwa miaka mingi.
Kwa mkoa
wa Tanga, unaojulikana kwa utajiri wa madini ya viwandani na ujenzi, mchanga
safi unaopatikana baada ya kuoshwa sasa ni malighafi yenye thamani kubwa kwa
viwanda vya saruji, miradi ya kimkakati ya Serikali ikiwemo Bandari ya Tanga na
ujenzi wa Bomba la Mafuta la EACOP katika Kata ya Chongeleani.
Teknolojia
hiyo pia inaelezwa kutoa fursa kwa wachimbaji wadogo na wawekezaji kuongeza
mapato, kwa kuuza bidhaa iliyoongezewa thamani badala ya mchanga ghafi ambao
unakuwa na bei ndogo ikilinganishwa na mchanga uliosafishwa.
Akizungumza
na Madini Diary, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa Tanga Mhandisi Laurent Bujashi
alieleza kuwa mchanga huo umeleta manufaa makubwa katika sekta ya viwanda na
ujenzi mkoani humo.
“Mchanga
unaosafishwa kiwandani hapa umetumika katika miradi mikubwa ya kimkakati
ikiwemo ukarabati wa Bandari ya Tanga, ujenzi wa baadhi ya viwanda mkoani hapa,
pamoja na utekelezaji wa bomba la mafuta ghafi kutoka Chongeleani, Tanga. Hatua
hii si tu kwamba imerahisisha upatikanaji wa malighafi zenye ubora, bali pia
imefungua soko jipya kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa mchanga,” alisitiza
Bujashi.
Kwa
upande wake, Afisa Uendeshaji wa kampuni hiyo, Kaparata Maulid, alieleza kuwa
mchanga unaosafishwa una mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya mkoa na
taifa kwa ujumla:
“Kupitia
teknolojia hii tumefanikisha kutoa mchanga wenye ubora wa hali ya juu unaokidhi
mahitaji ya miradi mikubwa ya kimkakati nchini. Hii ni hatua muhimu katika
kuongeza thamani rasilimali zetu na kuunga mkono jitihada za Serikali za
kujenga uchumi wa viwanda,” alisema Kaparata.
Alitaja
baadhi ya faida za mchanga unaosafishwa kuwa ni pamoja na kuboresha ubora wa
malighafi kwa miradi mikubwa ya miundombinu, kusaidia ujenzi wa viwanda vipya
na ukarabati wa miradi, kutengeneza ajira kwa wakazi wa eneo husika sambamba na
kutoa fursa ya soko endelevu kwa wachimbaji wadogo.
Kwa
uwekezaji huo, Tanga inajipambanua kama kitovu cha uvumbuzi na thamani katika
Sekta ya Madini, ikichangia moja kwa moja kwenye dira ya Tanzania ya kujenga
uchumi shindani wa viwanda kupitia malighafi
zinapatikana ndani ya nchi.
0 Maoni