Ikiwa ni
sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Siku ya
Upandaji Miti Kitaifa, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa
kushirikiana na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Wilaya ya
Masasi wamezindua rasmi kampeni ya upandaji miti katika eneo la Kanisa la KKKT
Masasi Mjini.
Katika
uzinduzi huo wiki hii, miti ya kivuli na matunda ilipandwa kuzunguka eneo la
kanisa kama hatua ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kuongeza thamani ya
mazao ya misitu kwa maendeleo endelevu.
Mgeni rasmi
katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mheshimiwa Lauteri Johni Kanoni,
aliipongeza KKKT Masasi kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika uhifadhi wa
mazingira kupitia upandaji wa miti. Alisisitiza kuwa miti ina mchango mkubwa
kwa maisha ya binadamu na kutoa wito kwa taasisi nyingine za kidini na kijamii
kuunga mkono juhudi hizo.
Kwa upande
wake, Mkuu wa Jimbo la Magharibi (Masasi) la KKKT, Mchungaji Wayzimen Simwinga,
aliwataka waumini na wananchi kwa ujumla kuheshimu uumbaji wa Mungu kwa kutunza
miti. Alieleza kuwa miti ni chanzo cha hewa safi ya oksijeni na hivyo, ukataji
miti holela unapaswa kudhibitiwa kwa kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika.
Aidha,
Mheshimiwa Kanoni aliipongeza TFS kwa mchango wake wa kugawa miche ya miti kwa
wadau mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha jamii kushiriki katika
uhifadhi wa misitu.
Maadhimisho
ya kilele cha Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji Miti Kitaifa
yanatarajiwa kufanyika Ijumaa, Machi 21, 2025, katika Uwanja wa Sabasaba,
Halmashauri ya Njombe Mji, mkoani Njombe. Kauli mbiu ya kitaifa kwa mwaka huu
ni:
“Ongeza
Thamani ya Mazao ya Misitu kwa Uendelevu wa Rasilimali kwa Kizazi Hiki na
Kijacho.”
Kwa upande wa
dunia, maadhimisho yanaongozwa na kauli mbiu: "Misitu na Chakula.”
Tukio hili
linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa misitu
na mchango wake katika usalama wa chakula, afya na maendeleo endelevu kwa
kizazi cha sasa na kijacho.
0 Maoni