Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania (TFS) pamoja na halmashauri za Mkoa wa Pwani wametakiwa kutumia mvua
zinazoendelea kunyesha nchini kushiriki kikamilifu katika kampeni ya upandaji
miti ili kufikia lengo la kupanda miti 13.5 milioni kwa mwaka.
Wito huo umetolewa na Mkuu
wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani
katika uzinduzi wa Siku ya Upandaji Miti uliofanyika katika Shule ya Msingi
Chalinze Mzee, ambapo jumla ya miti 560 ilipandwa.
Ndemanga alisema kila halmashauri
inapaswa kupanda miti takribani milioni 1.5 kwa mwaka, na kusisitiza umuhimu wa
kuhakikisha miti hiyo inatunzwa ili kudhibiti upotevu wa rasilimali.
“Uwiano kati ya miche
tunayopanda na ile inayokomaa bado hautoshelezi. Hatuwezi kuendelea kutumia
rasilimali nyingi kupanda miti ambayo haifuatiliwi wala kutunzwa. Ni lazima
tuhakikishe miti tunayopanda inakuwa,” alisema.
Kwa upande wake, Kamanda wa
TFS Kanda ya Mashariki, Mathew Ntilicha, akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa
Uhifadhi, Profesa Dos Santos Silayo, alisema upandaji miti ni sehemu ya juhudi
za kuhamasisha jamii kushiriki katika uhifadhi wa misitu kwa manufaa ya sasa na
ya vizazi vijavyo.
Alibainisha kuwa maadhimisho
ya Siku ya Upandaji Miti hufanyika Machi 21 kila mwaka, ambapo kwa mwaka 2025
yanaongozwa na kaulimbiu:
“Ongeza Thamani ya Mazao ya
Misitu kwa Uendelevu wa Rasilimali za Misitu kwa Kizazi cha Sasa na Kijacho.”
Akizungumza katika hafla
hiyo, Afisa Misitu wa Mkoa wa Pwani, Pierre Protas, alisema licha ya umuhimu
mkubwa wa misitu kwa jamii, bado kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta
hiyo.
“Changamoto tunazokabiliana
nazo ni pamoja na uanzishaji wa makazi na mashamba katika maeneo ya misitu,
utegemezi mkubwa wa kuni na mkaa kama vyanzo vya nishati na kipato kwa jamii, pamoja
na uhaba wa watumishi katika sekta ya maliasili,” alisema.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Chalinze ambaye pia ni Afisa Elimu Msingi, Miriam Kihiyo,
aliwataka walimu wakuu kuhakikisha kila mwanafunzi anapanda na kutunza mti,
ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutunza mazingira. Alisema zaidi ya wanafunzi
61,000 wanatarajiwa kushiriki.
Aidha, aliomba TFS kusaidia
upatikanaji wa dawa za kuzuia mchwa wanaoshambulia miti hiyo.
0 Maoni