Naibu Waziri Mkuu na Waziri
wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Mawakili wa Serikali kufanya kazi
kwa kuzingatia taaluma na haki ili kusaidia Watanzania sambamba na kuwa
washauri wazuri kwa viongozi wao.
Dkt. Biteko amesema hayo leo
Aprili 15, 2025 jijini Dodoma wakati alipofungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama
cha Mawakili wa Serikali.
“Ombi langu kwenu Mawakili
wa Serikali fanyeni kazi yenu kwa kuzingatia taaluma yenu ya sheria na haki, ni
wajibu wenu kushauri kwa haki na fanyeni kazi bila kuogopa,” amesema Dkt.
Biteko
Amesisitiza “Fanyeni kazi ya
kutetea Serikali yenu, nendeni mkaishauri Serikali na wakati wote mkatende
haki, ifanyeni haki kuwa rafiki yenu na anayetokea mbele yenu aone haki
imetendeka hata watakaopotoka wakihukumiwa waone wanastahili hukumu
waliyopewa,”
Halikadhalika Dkt. Biteko
amewapongeza Mawakili hao wa Serikali
pamoja na wadau mbalimbali kwa kuunda na kuendesha Kamati za Ushauri wa
Kisheria za Mikoa na Wilaya pamoja na kuendesha Kliniki za Ushauri wa Kisheria
bila malipo katika mikoa mitatu ya Dodoma, Kilimanjaro na Mwanza.
Vilevile, amesema kuwa
Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na Asasi za Kiraia, na binafsi katika
kuwahudumia wananchi kupata huduma za kisheria. Ametaja asasi na vyama hivyo
kuwa ni pamoja na Chama cha Wanasheria
Tanganyika (Tanganyika Law Society), Legal and Human Rights Centre (LHRC),
Tanzania Legal Aid Providers (TANLAP), Legal Service Facility (LSF), Tanzania
Human Rights Defenders Coalition (THRDC) pamoja na Watoa Huduma za Msaada wa
kisheria kama UNDP na UN Women.
Ametaja baadhi ya jitihada za Serikali katika kuboresha sekta ya sheria
nchini kuwa kuajiri Maafisa Sheria, Mawakili wa Serikali pamoja na Mahakimu na
imekuwa ikiwawezesha watoa huduma za kisheria kwa kuanzisha Huduma za Msaada wa
Kisheria, uanzishwaji wa Kamati za Ushauri wa Kisheria, Kliniki za Ushauri wa
Kisheria pamoja mafunzo kwa wataalamu wa sheria, ujenzi wa maeneo ya kutolea
huduma za kisheria kwa lengo la kuhakikisha huduma bora inawafikia wananchi.
Katika hatua nyingine, Dkt.
Biteko amemuelekeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kushughulikia changamoto
mbalimbali za Chama hicho cha Mawakili
wa Serikali ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kupata eneo la kujenga Makao Makuu ya
Chama na Vivutio vya Mafunzo kwa Mawakili wa Serikali katika mikoa ya Arusha na
Dodoma
Kwa upande wake, Waziri wa
Habari, Utamaduni. Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Palamagamba Kabudi amesema kuwa
Rais Mhe. Dkt. Samia ameimarisha sekta
ya sheria kwa kutekeleza masuala mbalimbali mfano kusaidia uwepo wa haki jinai na Kampeni ya Msaada wa Sheria ya Mama Samia.
Mhe. Kabudi amesema kuwa
umuhimu wa mkutano huo wa Mawakili wa Serikali kuwa ni kutoa fursa kwao ya
kukutana na kujadiliana masuala ya kitaaluma, maslahi yao pamoja na
kufahamiana.
Amewapongeza waasisi wa
Chama hicho kwa kujenga taswira nzuri huku akiwaasa viongozi wengine watakao
fuata kuendeleza taswira hiyo na amewataka
mawakili hao kuwa marafiki wa Mungu badala ya Mahakama kwa kutenda haki
na kusema kweli wakati wa kutimiza majukumu yao.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Hamza Johari amemshukuru Rais Samia
kwa kuendelea kukilea chama hicho kwa miaka mitatu na kusema kuwa ni wajibu wao
sasa kukilinda na kuhakikisha kinafikia malengo yake.
Pia, amebainisha kuwa
kupitia mkutano huo wameidhinisha Mpango Mkakati wa Chama hicho kitakachoufuata
na kutekeleza katika kipindi cha miaka mitano.
“Tumetengeneza Mpango
Mkakati tunaokwenda kuutekeleza kwa shauku kubwa pamoja na viongozi wapya
watakao chaguliwa katika Uchaguzi unaofanyika leo,” amesema Mhe. Johari.
Amesema hadi kufikia Aprili
9, 2025 idadi ya Mawakili wa Serikali waliojisajiliwa katika Daftari la
Mawakili wa Serikali imefikia 3,760 kutoka 2,652 waliosajiliwa wakati wa
kuanzishwa kwa Chama hicho.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Zanzibar, Mhe. Dkt. Mwinyi Talib Haji amewaomba
Mawakili na Maafisa Sheria wa Serikali kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia sheria ili kujenga jamii imara na
kupunguza mizozo katika jamii.
Aidha, amesema taasisi za sheria
ziendelee kushirikiana ili kusaidia wananchi na kuunga mkono jitihada za Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa
Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi za kuhudumia jamii na kuleta ustawi kwa
mustakabali kwa maendeleo ya nchi.
Rais wa Chama cha Mawakili
wa Serikali, Amedeus Shayo amesema kuwa Chama chao kimefanikiwa kujenga mfumo wa kielektoniki wa
kukusanya ada kwa wanachama pamoja na kuimarisha ushirikiano na taasisi
zinazoshughilika na masuala ya sheria za ndani na nje ya nchi.
“ Rais Samia ameendelea kuwa
kielelezo kizuri cha haki kupitia Kampeni yake ya Msaada wa Kisheria na Mawakili wanashiriki kutoa huduma za
sheria kwa wananchi. Pia, agizo la Rais Samia la Mawakili kuwa walinzi wa uchumi
wa nchi kwa kutumia kalamu limeweka msingi wa Chama hiki na umesaidia kuboresha
sheria kadhaa mfano Sheria ya Uwekezaji,” amesema Shayo.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Mstaafu na Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amemshukuru Rais
Mhe. Dkt. Samia kwa kuzindua Chama hicho mwaka 2022 na kusema “ Chama hiki kama
kilivyoanzishwa na malengo yake kitabaki kuwa Chama bora cha kitaaluma kwa
sababu Serikali na mawakili walijipanga kuwa nacho na hili ni jeshi la kulinda
uchumi wa nchi kwa sheria na kalamu,”
Mkutano huo uliohudhuriwa na
Mawakili wa Serikali kutoka katika Wizara, Wakala na Taasisi za Serikali, Mashirika ya umma umeongozwa na Kauli mbiu “ Utawala wa Sheria katika
Utekelezaji wa Majukumu ya Serikaki ni Nguzo Muhimu katika Kufikia Malengo ya
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”
0 Maoni