Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) inatarajia kuendelea kuimarisha huduma za utalii
katika mapango ya Amboni yaliyopo mkoani Tanga ili yaweze kuvutia watalii wengi
kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Akizungumza
na watumishi wa kituo hicho Kaimu Meneja wa Uhusiano kwa Umma wa Mamlaka hiyo,
Afisa Uhifadhi Mkuu Hamis Dambaya amesema kuwa malengo ya kuboreshwa kwa huduma
katika mapango ya Amboni yanatokana na mwelekeo mpya wa mamlaka hiyo ya kutaka
kuongeza mapato na kutanua wigo wa vivutio vya utalii.
“Ndani ya
Mapango tumeweka miundombinu ya taa, njia ya kutembelea wageni, mifumo ya
TEHAMA na mazingira ya kupumzika wageni wanaotembelea Mapango haya, barabara ya
kuja eneo la Mapango zinapitika vizuri na ujenzi wa geti umekamilika,
tutaendelea na jitihada mbalimbali za maboresho ili eneo hili livutie wageni
wengi zaidi,” alisema Dambaya.
Miongoni mwa
huduma zitakazoboreshwa katika eneo hilo ni pamoja na barabara ya kuingia
mapango hayo na uanzishwaji wa mazao mapya ya utalii.
Mapango ya
Amboni yaliyopo mkoani Tanga ni moja ya kivutio kikubwa cha utalii kutokana na
kuwepo kwa miamba ya asili ambayo inatokana na historia ya kuumbwa kwa dunia.
Kwa mujibu
wa Mkuu wa Hifadhi ya Mapango ya Amboni Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza
Ramadhan Rashid, eneo hilo hutembelewa na wastani wa wageni 18,000 kwa mwaka
huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka kutokana na uboreshaji wa miundombinu ya
utalii pamoja na mifumo ya malipo.




0 Maoni