Mkutano wa
20 wa Kawaida wa Waratibu wa Kitaifa wa Nchi za Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa
Makuu (ICGLR) umefanyika tarehe 10 Novemba, 2025 jijini Kinshasa, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo - DRC.
Mkutano huo
ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje (RIMC) pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali
(SUMMIT) wa Jumuiya hiyo iliyopangwa kufanyika Novemba 13 na 15, 2025 mtawalia.
Mkutano huo
umefunguliwa na Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda wa DRC, Mhe. Floribert
Anzuluni Isiloketshi ambapo pamoja na masuala mengine, amewasihi waratibu hao
kutumia mkutano huo kuja na mapendekezo yatakayoboresha utendaji kazi wa
Sekretarieti ya Maziwa Makuu ili iweze kutekeleza kwa ufanisi zaidi majukumu
yake ya msingi, ikiwemo kuleta amani, usalama na maendeleo katika nchi 12
Wanachama wa Jumuiya hiyo.
Tanzania
ikiwa moja ya nchi waasisi wa ICGL, inashiriki mkutano huo kikamilifu ambapo
Mratibu wa Kitaifa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika kutoka Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Ellen Maduhu ameongoza
ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo.
Naye, Katibu
Mtendaji wa ICGL, Balozi João Samuel CAHOLO amesema, licha ya mafanikio ambayo
Sekretarieti hiyo imepata chini ya uongozi wake, bado jitihada zaidi
zinahitajika kuhakikisha amani ya kudumu na usalama vinapatikana katika Ukanda
huo hususan katika nchi za DRC, Jamhuri ya Sudan, Jamhuri ya Sudan Kusini na
Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Amehusisha
umasikini, ukosefu wa usawa na wananchi kutozifikia rasilimali za nchi zao kuwa
ni baadhi ya vyanzo vya migogoro barani Afrika, na kutoa wito wa kukomesha
migogoro kwa kuvishugulikia vyanzo vyake.




0 Maoni