WAZIRI MKUU,
Kassim Majaliwa amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan madarakani ameweza kutekekeza miradi yote ya kimkakati
iliyoasisiwa na watangulizi wake ikiwemo ya Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe
Magufuli.
Amesema kuwa
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ametimiza ahadi aliyoitoa kwa Watanzania mara
alipoingia madarakani ya kuwa hakuna mradi utakaosimama chini ya uongozi wake
na kwamba ataendeleza kila kilichoanzishwa na watangulizi wake.
Amesema hayo jana Jumanne (Machi 18, 2025) alipozungumza katika Kongamano la kumpongeza
Mheshimiwa Rais DKt. Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio ya miaka minne ya
uongozi wake lililoandaliwa na Waandishi
wa Habari Mahiri wa Mkoa wa Mwanza kwenye ukumbi wa Tunza jijini Mwanza.
Mheshimiwa
Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia
alipotoa hotuba yake ya kwanza bungeni
aliahidi kuwa miradi yote itaendelezwa na mingine mipya itaanzishwa.
Mheshimiwa
Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia amefanikiwa kusimamia kwa karibu utekelezaji
wa miradi mikubwa ya maendeleo pamoja na ya huduma za jamii inayowagusa
wananchi wote hadi vijijini kwenye sekta za afya, elimu na maji “wote ni
mashahidi wa mafanikio makubwa ambayo yamefikiwa na Serikali katika utekelezaji
wa miradi hiyo.”
Kuhusu sekta
ya maji Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa hivi sasa Serikali inatekeleza miradi
kwenye maziwa, mito na Mabwawa kwa ajili ya kuwapelekea wananchi wenye uhitaji
wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini.
Aliitaja
mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Tabora, Singida, Dodoma na Mara kuwa
itakayonufaika na miradi wa maji ya Ziwa Victoria Alisema miradi kama hiyo iko pia katika mikoa
ya Geita na Kagera.
Kuhusu afya
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imewekeza katika miundombinu ya kutolea
huduma za afya, dawa na vifaa tiba kuanzia ngazi ya kata hadi Taifa, lengo likiwa ni kusaidia
kupunguza adha kwa wananchi kutembea umbali mrefu kupata huduma za afya ikiwemo
za kibingwa.
Kuhusu
nishati ya umeme amesema wilaya na vijiji vyote vimepatiwa umeme na hivi sasa
Serikali inasambaza umeme kwenye vitongoji na visiwa ili kuhakikisha kwamba kila
nyumba anamoishi Mtanzania inafikiwa na huduma ya umeme.
Akizungumzia
kilimo Mheshimiwa Majaliwa amesema zao la pamba ambalo awali uzalishaji wake
ulikuwa umezorota Serikali imeimarisha mifumo ya masoko ya zao hilo kwa
kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umepandisha bei ya zao kilo.
Amesema hivi
sasa zao la hilo limerudi kwenye nafasi yake ya kuwa moja kati ya mazao
makuu ya biashara nchini na viwanda
vingi vya kuchambua pamba vimejengwa
hasa mkoani Simiyu.
Kuhusu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuteuliwa kuwa
mgombe wa Urais wa CCM Katie uchaguzi mkuu ujao, Mheshimiwa Majaliwa amesema
kuwa amefurahishwa na kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Mwanza Michael Lushinge kuwa mkoa huo
utaongoza tena kwa kumpiga kura nyingi za ndiyo mgombea Urais wa CCM.
Akitoa mada
katika kongamano hilo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Masanja Kagosa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan alianzia Kanda ya Ziwa kwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR ya kutoka
Mwanza kwenda Isaka lengo likiwa ni kuifanya Mwanza kuwa kitovu cha biashara
kwa Ukanda wa Maziwa Makuu.
Naye Mratibu
wa kongamano hilo, Aloyce Nyanda amesema kuwa
kwa namna yoyote kazi zinazofanywa na Serikali zina manufaa makubwa kwa
wananchi ndiyo maana yeye na waandishi wenzake wa habari wameamu kujadili
mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa
Rais Dkt. Samia kama kiongozi wa
mkuu wa nchi na mtumishi wa watu.
0 Maoni