WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wadau wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi
nchini watoe mafunzo yanayozingatia mahitaji halisi ya soko la ajira.
“Mahitaji ya
soko la ajira tutayajua kwa kufanya tafiti za mara kwa mara kwa ushirikiano
kati ya Serikali, sekta binafsi, na mashirika ya kimataifa.”
Ametoa wito
huo leo (Jumanne, Machi 18, 2025) katika Maadhimisho ya miaka 30 ya Uanzishwaji
wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) yaliyofanyika katika
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Amesema
katika zama hizi zenye kasi ya maendeleo ya teknolojia, ni muhimu kwa VETA
kuendelea kujiimarisha kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia duniani.
“Toeni
mafunzo ya ufundi stadi yanayoendana na mabadiliko ya teknolojia, mafunzo hayo
yajumuishe ujuzi wa teknolojia za kisasa zinazochochea uzalishaji wenye tija.”
Akizungumza
kuhusu umuhimu wa Elimu ya Ufundi Stadi, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa
takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO) zinaonesha kuwa takribani asilimia 70
ya ajira zote ni ajira binafsi na kwa watu wenye elimu ya ufundi stadi hasa
kwenye sekta za kilimo, ujenzi, usafirishaji, na huduma za kijamii.
“Kwa upande
wa nchi yetu, takwimu za ajira zilizozalishwa kati ya mwaka 2020 na 2024
zinafikia Milioni 7 ambapo ajira binafsi katika sekta isiyo rasmi imeajiri watu
milioni 6.1 sawa na asilimia 87.1 ambapo wengi wao wana elimu ya ufundi stadi,
na sekta rasmi imeajiri watu 907,873 (asilimia 12.9) ambapo wengi wao ni wale
wenye elimu ya juu”.
Pia, Waziri
Mkuu ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi
ya Rais - TAMISEMI na Wizara ya Viwanda na Biashara wahakikishe ujenzi wa vyuo
65 vya ufundi unakamilika haraka.
Waziri Mkuu
amesema ukamilishwaji wa vyuo hivyo vinavyojengwa na Serikali unalenga kutimiza
dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha Watanzania
kiujuzi.
“Ujenzi wa
vyuo hivi ukikamilika, VETA itakuwa na vyuo 145 katika ngazi ya Mikoa yote 26
na Wilaya zote nchini. Vilevile, katika vyuo 80 vilivyopo, vyuo 30 vilikamilishwa
katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita (6). Tuna kila sababu ya
kumpongeza Rais wetu kwa kazi kubwa anayowafanyia Watanzania.”
Kadhalika
Waziri Mkuu ameitaka VETA ihakikishe inatangaza fursa za mafunzo zilizopo ili
vijana haswa wa vijijini waweze kuzitumia. “Inawezekana kabisa kuwa, wapo
vijana katika maeneo mbalimbali nchini haswa ya vijijini ambao hawana taarifa
ya fursa za mafunzo zilizopo.”
0 Maoni