Serikali imetoa onyo
kwa watu na kampuni zinazoendelea kuzalisha bidhaa za mifuko ya plastiki
iliyopigwa marufuku na kuingiza katika matumizi kwa njia za panya.
Imesema itaendelea
kufanya doria za kushtukiza katika viwanda, viwanda bubu na masoko ili
kuwabaini na kuwachukulia hatua wahusika wote wanaojihusisha na biashara hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema
hayo leo Mei 27, 2025 jijini Dodoma wakati akitoa tamko la Serikali kuelekea
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kilele chake kitakuwa jijini
Dodoma na mgeni rasmi anatarajia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hatua hiyo inakuja
kutokana na kujitokeza kwa changamoto ya matumizi ya vifungashio vya plastiki
aina ya tubings kutumika kama vibebeo na vifungashio ambavyo havina sifa na
kutokukidhi matakwa yaliyowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Kufuatia hatua hiyo
Mhandisi Masauni amelielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC), Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mamlaka nyingine za umma
kuendelea kufuatilia na kuwabaini wahusika wote wanaokiuka sheria na kuzalisha
bidhaa za plastiki zilizopigwa marufuku kuzalishwa na kutumika nchini.
“Niwakumbushe
Watanzania wenzangu kuzingatia maelekezo ya Serikali kuachana na mifuko ya
plastiki na kutumia mifuko mbadala ambayo kwa sasa inapatikana nchini kote kwa
gharama nafuu” amesisitiza Mhandisi Masauni.
Aidha, amesema kuwa
pamoja na changamoto hiyo, kwa kiasi kikubwa Tanzania imepiga hatua katika
kudhibiti taka za plastiki baada ya kupiga marufuku uzalishaji, uingizaji,
usambazaji na matumizi ya mifuko ya plastiki kuanzia Juni, 2019, hatua
iliyosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Ili kuhakikisha
wananchi wanapata uelewa kuhusu kutambua mifuko na vifungashio vya plastiki
vilivyoruhusiwa, Waziri Masauni amesema kuwa Serikali imeendelea kutoa elimu
kwa umma sambamba na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uzalishaji wa
mifuko mbadala ambazo ni rafiki kwa mazingira.
Waziri Masauni
amesema Kutakuwa na Kongamano la Vijana litakalowatanisha vijana mbalimbali
wakiwemo wanafunzi wa vyuo, wajasiriamali na mabalozi wa mazingira
litakalofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 3 Juni, 2025.
Kwa mujibu wa
Mhandisi Masauni, Kaulimbiu ya madhimisho ya mwaka huu ni ‘Tanzania Ijayo
Tuwajibike Sasa, Dhibiti Matumizi ya Plastiki’ inayolenga kuikumbusha jamii
kuwa mazingira na rasilimali zake ni msingi wa uhai na maisha pamoja na ukuaji
wa Uchumi, hivyo utunzaji na uhifadhi wa mazingira na rasilimali
zake ni jambo muhimu.
0 Maoni