Mkoa wa Dar es Salaam
umeendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kupitia
Sekta ya Madini kwa mwaka wa fedha 2024/2025, baada ya kufanikisha makusanyo ya
Shilingi Bilioni 23.02 kufikia mwezi Mei, sawa na asilimia 125 ya lengo la mwaka.
Ofisi ya Afisa Madini
Mkazi wa Mkoa huo ilipangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 18.36, lakini hadi
kufikia Machi mwaka huu tayari ilikuwa imetimiza lengo hilo, na sasa imevuka
kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza jijini
Dar es Salaam, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa huo, Mjiolojia Lameck Gabote amesema
mafanikio hayo yametokana na usimamizi thabiti wa vyanzo mbalimbali vya
maduhuli ikiwemo mrabaha, ada na tozo mbalimbali.
“Mwaka ujao wa fedha
2025/2026 tumepangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 24. Tuna imani kubwa kwamba
tutafikia na kuvuka lengo hilo. Mkoa wa Dar es Salaam uko ‘active’ kukusanya
maduhuli, hatulali,” amesema Gabote kwa msisitizo.
Ameeleza kuwa licha
ya Dar es Salaam kutokuwa na shughuli kubwa za uchimbaji wa madini, imekuwa
kitovu muhimu cha biashara ya madini kutokana na uwepo wa Soko la Kimataifa la
Madini, bandari na uwanja wa ndege wa kimataifa ambavyo hurahisisha biashara ya
madini ndani na nje ya nchi.
Aidha, Gabote
amebainisha kuwa ofisi yake pia inasimamia mgodi mdogo wa dhahabu uliopo kijiji
cha Kibindu, Handeni mkoani Tanga, ambao uzalishaji wake ni mdogo – ukitoa
wastani wa gramu 12 hadi 25 kwa mwezi.
Kwa mujibu wa Gabote,
mikoa ya Dar es Salaam na Pwani imejaliwa kuwa na aina mbili za madini: madini
ya ujenzi na madini ya viwandani, ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa
makusanyo ya maduhuli. Madini haya yamekuwa yakitumika katika miradi mikubwa ya
maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara ya BRT unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Takwimu hizi
zinaonesha ukuaji chanya wa Sekta ya Madini katika maeneo yasiyokuwa ya
uchimbaji wa moja kwa moja, na kuonesha umuhimu wa miundombinu ya biashara kama
masoko, bandari na viwanja vya ndege katika kuchochea maendeleo ya sekta hiyo.
0 Maoni