WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa ameshuhudia utiaji saini wa hati ya makubaliano ya ujenzi wa kituo
kikubwa cha kupandikiza figo pamoja na utoaji mafunzo kwa madaktari bingwa
ambacho kitakuwa ni kikubwa katika ukanda wa Jangwa la Sahara.
Kituo hicho ambacho
kitajengwa kwenye Hospitali ya Kanda ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma ni
ushirikiano kati ya Shirika la Tiba la TOKUSHUKAI, Hospitali ya Benjamin Mkapa
na Chuo Kikuu cha Dodoma na kinatarajia kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 28
ikiwa ni msaada usiokuwa na masharti yoyote.
Utiaji saini huo
umefanyika jana (Jumatatu, Mei 26, 2025) wakati kongamano la Biashara,
Uwekezaji na Utalii lililowakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na
wafanyabiashara na wawekezaji wa Japan katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya
Westin, Osaka, Japan, ikiwa ni sehemu ya
ushiriki wa Tanzania katika maonersho ya World Expo Osaka 2025.
Kongamano hilo lilifunguliwa na Mheshimiwa Majaliwa.
Akizungumza baada ya
utiaji saini huo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa, Profesa
Abel Makubi amesema wamesaini makubaliano na shirika hilo linaloundwa na kundi
la madaktari Wakijapan ambao wamekuwa wakisaidia utoaji na uboreshaji huduma za
afya. “Hawa ni wadau wetu wa muda mrefu na walikuwa watu wa kwanza kusaidia
utoaji wa huduma Dialysis katika hospitali ya Benjamin Mkapa.”
“MOU hii ambayo
tumeisaini sasa hivi ni kwa ajili ya kujenga kituo cha umahiri katika
upandikizaji figo kwenye eneo la Tanzania na Ukanda wa Jangwa la Sahara.”
Amesema mbali na
ujenzi wa kituo hicho ambacho kitajengwa ndani ya hospitali ya Benjamin Mkapa
na kutarajiwa kukamilika na kuanza kutoa huduma ndani ya miaka mitatu, pia
Serikali ya Tanzania imejipanga kusaidia baadhi ya maeneo ili kuhakikisha mradi
huo unakamilika kwa wakati. Ujenzi wa kituo hicho unarajiwa kuanza mwaka huu.
“Tunatoa shukurani
kwa Serikali ya Japan kupitia wadau hao na tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi ambayo yametufanya sisi tuweze
kufikia makubaliano na wadau hawa. Makubaliano haya yanakwenda kusaidia
wananchi kwa ajili ya kuboresha huduma za figo si kwa Watanzania tu bali kwa
Waafrika wengine.”
Profesa Makubi
amesema pia kituo hicho kitakuwa kinatoa mafunzo kwa ajili ya kupandikiza figo,
pamoja na kufanya tafiti kwa ajili ya kuzuia au kupunguza magonjwa
yanayohusiana na figo. Mafunzo yatolewa kwa ushirikiano kati ya Hospitali ya
Benjamin Mkapa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Kwa upande wake,
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Lugano Kusiluka amesema
makubaliano hayo yataimarisha huduma ya upandikizaji figo ambao unafanyika
katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma kwa ushirikiano wa wataalamu
wa hospitali hiyo pamoja na wa UDOM.
Amesema kwa sasa UDOM
ipo katika mchakato wa kuanzisha programu ya uhandisi wa vifaa tiba ili
kuounguza gharama kwa Serikali kutumia wataalam kutoka nje ya nchi kutengeneza
vifaa hivyo mara vinapoharibika. “Kwa makubaliano haya mbali na kufundisha
wataamu kutengeneza vifaa hivyo, pia watafundisha namna ya kuvitunza ili
visiharibike.”
Pia, Profesa Kusiluka
amesema katika makubaliano hayo Tanzania inakwenda kunufaika kwa kuwa kituo
kikubwa cha upandikizaji figo inachotarajiwa kujengwa kitatumika katika
kufundisha madaktari bingwa pamoja na wataalam kutoka mataifa mbalimbali ya
Afrika kupandikiza figo na baadae kupandikiza viungo vingine.
Hati nyingine
iliyosainiwa ni kati ya ushirikiano kati Chuo Kikuu cha Dodoma na Hospitali ya
Benjamin Mkapa na Chama cha Maendeleo na Uchumi Afrika cha Japan (AFRECO), hati
hizo ni sehemu ya hati sita za makubaliano zilizosainiwa leo kati ya Serikali
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
mashirika ya Japan.
0 Maoni