Mkuu wa Kitengo Cha
Mawasilino Serikali na Msemaji wa Wizara ya TAMISEMI, John Mapepele ametoa wito
kwa Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kutanguliza uzalendo na
weledi wakati wa utoaji wa taarifa ili habari hizo ziwe na tija kwa taifa.
Mapepele ametoa wito
huo mwisho wa juma wakati akiwasilisha
maada kuhusu Mawasilino ya Kimkakati ya Kutangaza Nafanikio ya Sekta za Afya,
Elimu na Miundombinu chini ya TAMISEMI kwa Maafisa Habari zaidi ya 200 wa Mikoa na Halmashauri zote
nchini jijini Dodoma kwenye kikao kazi cha siku mbili kwa MaafisaHabari hao
kilichoratibiwa na Wizara hiyo.
Kikao kazi hicho
kilichofunguliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI
Mhe.Mohamed Omary Mchengerwa na kufungwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari
Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa
kimejadili pamoja na mambo mengine, mikakati mbalimbali ya kutangaza mafanikio
ya Serikali, pia kuwajengea uwezo Maafisa Habari hao kwa mada mbalimbali za
kitaaluma hususan matumuzi ya mifumo ya kidigitali kwenye utoaji wa taarifa na
kuja na maazimio kadhaa ya kuboresha utendaji kazi.
Aidha, Mapepele
amesema kumekuwa na mafanikio makubwa katika miradi ya maendeleo ambayo
imetekelezwa katika mikoa na Halmashauri zote nchini ambayo haijatangazwa
ipasavyo na Maafisa Habari katika maeneo hayo
na kuwataka kuwa wabunifu wa kutoa taarifa hizo.
"Ndugu zangu
Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya mapinduzi makubwa kwenye sekta ya miundombinu ambapo tumeshuhudia
mabarabara, madaraja, vituo vya mabasi na masoko yakitengenezwa kila uchao,
ukiachia mbali madarasa, zahanati, vituo vya afya na vifaa tiba kwenye kila
kona hivyo ni wajibu wetu sisi Maafisa Habari wa Halmashauri na Mikoa kuwa
wazalendo na kuisemea Serikali yetu ili wananchi waweze kujua na kutumia huduma
hizi kikamilifu". Amefafanua Mapepele.
Akifungua kikao kazi
hicho Mhe. Mchengerwa amewataka Maafisa
Habari wote wa TAMISEMI kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi kwa wakati
za utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali katika maeneo yao ya kazi.
"Mmebeba dhamana
kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi hivyo msiache watanzania
walishwe habari potofu," amesisitiza Mhe. waziri Mchengerwa.
Akifunga kikao kazi
hicho, Katibu Mkuu Msigwa ameipongeza Wizara ya TAMISEMI kwa kuratibu kikao
kazi hiki ambapo ameshauri kiwe
kinafanyika kila mwaka ili kufanya tathmini wa utendaji wa kazi na kujadiliana
masuala mbalimbali ya utendaji wa kazi wa kundi hili kubwa la Maafisa Habari wa
Mikoa na Halmashauri nchini katika kutoa taarifa za miradi ya maendeleo.
Mara baada ya
kumalizika kikao kazi hiki, Maafisa
Habari hao walipata fursa ya kutembelea Mji wa Serikali wa Mtumba na kujionea
kukamilika kwa Mji huo.
0 Maoni