MAKUSANYO ya
maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Madini katika Mkoa wa Kagera yatokanayo
na mrabaha, tozo na ada mbalimbali kwa mwaka wa fedha ulioanza Julai 2024/ 2025
ni Shilingi Bilioni 3.2.
Kagera ilipangiwa
kukusanya Shilingi Bilioni 5.8 na mpaka mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu
wa 2025 wamefanikiwa kukusanya kiasi hicho cha fedha kikiwa ni sawa na asilimia
82 ya lengo katika kipindi cha miezi nane.
Akizungumza
Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kagera, Nobert Mkopi amesema fedha hizo
zimekusanywa kutokana na jitihada mbalimbali walizofanya katika usimamizi wa
Sekta ya Madini katika halmashauri zote saba za Mkoa wa Kagera.
“Mkoa wa
Kagera kwa maana Sekta ya Madini
tunasimamia halmashauri zote saba kwa
maana ya wilaya za Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Muleba, Bukoba, Biharamulo na
Ngara, kuna shughuli mbalimbali za
uchimbaji madini,”amesema Mkopi na
kuongeza.
“Mkoa huu
yanapatikana madini mbalimbali ikiwemo Bati, Dhahabu, Nickel, Wolframite (WO3),
Madini ya Viwandani na Madini Ujenzi".
“Maeneo ya
Kyerwa yanachimbwa madini ya bati, yanachimbwa kihalali kwa leseni za uchimbaji
mdogo lakini pia kuna leseni kubwa ya utafiti na madini haya yanachangia
asilimia 32 mpaka sasa ya maduhuli tuliyokusanya ya Shilingi Bilioni 3.2 na
fedha nyingine zinatoka kwenye madini mengine ikiwemo dhahabu na ada mbalimbali
za vibali na leseni," amesema Mkopi.
Aidha,
amesema mwenendo wa ukusanyaji maduhuli
sio mbaya na hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha wana
imani watafikia lengo lililokusudiwa.
Katika hatua
nyingine, Mkopi ametoa wito kwa wawekezaji kote nchini kuchangamkia fursa za
uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini mkoani Kagera ambao una utajiri
mkubwa wa madini mbalimbali ikiwemo Bati, Dhahabu, Nickel, Wolframite (WO3),
Madini ya Viwandani na Madini ujenzi.

0 Maoni