Kamishna wa
Uhifadhi - TANAPA, Musa Juma Kuji jana Machi 18, 2025 alifanya kikao kazi na
Wakuu wa Hifadhi za Taifa zote 21 Jijini Dodoma kwa lengo la kufanya tathmini
ya hali ya uhifadhi na utalii pamoja na kupokea ushauri na maoni ya namna bora
ya kuboresha utendaji kazi katika Hifadhi za Taifa.
Akizungumza
katika kikao hicho Kamishna Kuji aliwasisitiza Wakuu wa Hifadhi za Taifa nchini
kuongeza jitihada katika utendaji kazi ili kuboresha ukuaji wa utalii pamoja na
kuongeza mapato kwa Taifa.
“Tuendelee
kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa tunabuni mazao mapya ya utalii ambayo
yatakuwa na matokeo ya kuongeza mapato ndani ya shirika na serikali kwa ujumla.
Pia, nakubaliana na ushauri wenu wa kuongeza nguvu ya kuyafikia masoko ambayo
yanaongoza kuleta watalii wengi wanaotembelea Hifadhi za Taifa,” alisema
Kamishna Kuji.
Wakuu wa
Hifadhi za Taifa walimpongeza Kamishna Kuji kwa namna anavyoendelea kujitoa na
kuwafikia maafisa na askari wa Uhifadhi katika maeneo yao ya kazi kwa kufanya
nao vikao, kuwasikiliza na kuwatia moyo jambo ambalo limekuwa likileta tija kwa
watumishi na kuwaongezea morali ya kazi.
“Afande
Kamishna tunakushukuru na kukupongeza sana kwa uamuzi wako wa kufanya ziara za
kutembelea hifadhi na kukutana na maafisa na askari katika vituo vyao kwani
jambo hilo limesaidia sana kutatua changamoto zilizopo. Hivyo watumishi
wamekuwa wakipata faraja na kuongeza morali ya utendaji kazi, hongera sana
afande”. alisema Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Charles Ngendo, Mkuu wa Hifadhi
ya Taifa Rumanyika-Karagwe.
Aidha, Wakuu
wa hifadhi hao walipata fursa ya kujadili masuala muhimu ambayo yamelenga
kuboresha utendaji kazi pamoja na kuinua kiwango cha utoaji huduma kwa watalii
wanaotembelea Hifadhi za Taifa Tanzania.
Shirika la
Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) linasimamia jumla ya hifadhi 21 ambazo kila
hifadhi ina Mkuu wa hifadhi ambaye ni Afisa wa cheo cha juu cha maamuzi ya
mwisho kwa ngazi ya hifadhi husika na ni kiungo muhimu sana katika usimamizi na
uratibu wa shughuli za uhifadhi na utalii nchini.
Na. Andrew Mbai
- Dodoma



0 Maoni