Tume ya Madini imesema kuanzishwa kwa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini kumeongeza uwazi katika biashara ya madini na kusaidia kudhibiti utoroshaji wa rasilimali hiyo, hatua iliyochangia kuongezeka kwa mapato ya Serikali.
Akizungumza leo katika
Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya
Chinangali jijini Dodoma, Afisa wa Tume ya Madini kutoka Kurugenzi ya
Ukaguzi na Biashara ya Madini, Ibrahim Akyoo, amesema mfumo huo
umewezesha wachimbaji na wafanyabiashara kuuza madini kupitia njia
rasmi na hivyo kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo.
Amesema kwa
sasa nchini kuna masoko ya madini 44 na vituo vya ununuzi wa madini
120 vinavyorahisisha biashara ya madini na kuhakikisha Serikali
inapata mapato stahiki yatokanayo na rasilimali hizo.
Akyoo
amesema miongoni mwa majukumu ya Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya
Madini ni kusimamia biashara ya madini nchini, kuhakikisha ushiriki
wa Watanzania katika sekta hiyo unaongezeka, kudhibiti utoroshaji wa
madini, kufanya ukaguzi wa fedha na kodi pamoja na kutoa huduma za
kimaabara kwa wadau wa sekta hiyo.
Amesema kupitia maonesho
hayo, Tume ya Madini inaendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau
kuhusu fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya madini, zikiwemo
biashara ya madini, uchimbaji, uongezaji thamani, utoaji wa huduma na
shughuli nyingine katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
Amesema
hatua hizo zinaendelea kuifanya sekta ya madini kuwa miongoni mwa
sekta muhimu zinazochangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa.

.jpeg)

0 Maoni