Na. Brigitha Kimario- Arusha
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limepokea tuzo ya Mifumo ya Taarifa za Kijiografia (GIS) kwa Ukanda wa Africa kutoka Esri Eastern Africa, baada ya kutambuliwa kwa umahiri wake katika matumizi ya teknolojia ya ArcGIS katika shughuli za uhifadhi na utalii.
Akikabidhi tuzo hiyo leo Juni 18, 2026 Mwakilishi wa Esri Eastern Africa na Meneja wa Mafanikio kwa Wateja (Customer Success Manager), Bi. Monica Mwanzia, alisema TANAPA imeibuka mshindi kutokana na matumizi bora ya teknolojia ya GIS katika ukusanyaji wa taarifa za uwandani (spatial data collection), kuchakata (spatial analysis) na uandaaji wa ramani (map production).
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi
TANAPA, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara Massana
Mwishawa alisema kuwa ushindi wa tuzo hiyo ni uthibitisho wa
mafanikio makubwa ambayo TANAPA imeyapata katika matumizi ya
teknolojia za kisasa.
Kamishna Mwishawa alisema, “Ushindi
huo wa tuzo ya GIS kwa Ukanda wa Afrika ni heshima kwa Taifa na
TANAPA kwa ujumla ambao unatupa motisha na ari ya kuendelea kuwekeza
katika matumizi sahihi ya mifumo ya GIS ili kuendana na kasi ya
Maendeleo ya Sayansi na Tecknolojia Duniani.”
Aidha,
alibainisha kuwa TANAPA imeendelea kutumia teknolojia ya GIS kwa
zaidi ya miaka 15 tangu mwaka 2011, ambapo imekuwa ni nyenzo muhimu
katika kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya hifadhi na
maeneo jirani, kukusanya na kuchambua data za kijografia, kuongeza
ufanisi wa maamuzi ya kiutendaji na kuimarisha usimamizi wa
rasilimali za uhifadhi.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa
Uhifadhi na Mkuu wa Kitengo cha GIS TANAPA, Dkt. Abel Mtui, alisema
kuwa mfumo huo umeimarisha uwajibikaji na ufanisi kwa watumishi
wanaotekeleza majukumu yao uwandani.
Vilevile, Kamishna Mtui
aliongeza, “Teknolojia ya GIS inawezesha kufuatilia maeneo
yaliyokaguliwa, ukubwa wa maeneo yaliyofanyiwa doria, kubaini
mtawanyiko wa wanyamapori na kutambua maeneo yenye changamoto za
ujangili. Pia mfumo huo husaidia kutambua maeneo yenye fursa za
uwekezaji katika malazi ya watalii, miundombinu ya barabara na
viwanja vya ndege.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1959, TANAPA
imeendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia mbalimbali za kisasa
ikiwemo GIS, TEHAMA na mifumo mingine ya kidijitali inayotumika
katika shughuli za uhifadhi, utalii, ukusanyaji wa mapato na
manunuzi. Matumizi ya teknolojia hizo yameongeza kasi kwa TANAPA
kujizolea tuzo mbalimbali maarufu za kitaifa na kimataifa.



0 Maoni