Wakala ya Barabara za Vijijini na
Mijini (TARURA) imewakutanisha wahandisi na wataalamu wa sekta ya
barabara katika mafunzo maalum yanayolenga kuimarisha usalama wa
watumiaji wa barabara wakati wa usanifu, ujenzi na matengenezo ya
miundombinu ya barabara nchini.
Mafunzo hayo
yanayofanyika mkoani Morogoro yanalenga kuongeza uelewa na uwezo wa
wataalamu katika kuzingatia viwango vya usalama barabarani ili
kupunguza ajali na kulinda maisha ya watumiaji wote wa
barabara.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Mratibu
Msaidizi wa Mradi wa RISE, Mhandisi Lwitiko Mwandobo, amesema mafunzo
hayo yameandaliwa mahsusi kuwajengea uwezo wahandisi na kuwakumbusha
wajibu wao wa kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara
unazingatiwa tangu hatua ya usanifu hadi utekelezaji wa
miradi.
"Tunataka kuhakikisha kwamba kila mradi wa
barabara unazingatia usalama kwa kuweka alama zote muhimu,
miundombinu rafiki kwa watumiaji na hatua nyingine za kinga
zitakazosaidia kupunguza ajali zinazoweza kuepukika. Hii ni sehemu ya
juhudi za kulinda maisha ya wananchi na mali zao", amesema
Mhandisi Mwandobo.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA
mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Geofrey Mkinga amesema usalama wa
watumiaji wa barabara ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano wa
wadau wote ili kufikia lengo la kupunguza kwa kiwango kikubwa ajali
za barabarani na pia kuna umuhimu wa kuendelea kuimarisha mifumo ya
kisheria na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya
barabara.
"Tukizingatia usalama katika kila hatua
ya ujenzi wa barabara, kuimarisha elimu kwa umma na kuhakikisha
miundombinu inakidhi viwango vinavyotakiwa, tutapunguza kwa kiasi
kikubwa ajali za barabarani na madhara yake kwa jamii", amesema
Mhandisi Mkinga.
Naye, Mratibu wa Masuala ya Usalama
Barabarani kutoka (TARURA), Mhandisi Faizer Mbange, amesema mwelekeo
wa sasa katika ujenzi wa barabara unalenga kuhakikisha mahitaji ya
makundi yote ya watumiaji wa barabara yanazingatiwa ikiwemo waenda
kwa miguu, waendesha baiskeli, bodaboda, bajaji pamoja na watumiaji
wa vyombo vingine vya usafiri.
Amesema tofauti na
ilivyokuwa hapo awali ambapo usanifu wa barabara ulijikita zaidi
katika magari, sasa miundombinu ya barabara inapaswa kuwa jumuishi na
salama kwa kila mtumiaji bila kujali aina ya usafiri
anaotumia.
Mafunzo hayo yamewakutanisha wataalamu kutoka
taasisi mbalimbali za sekta ya barabara na usafiri zikiwemo Wakala wa
Barabara Tanzania (TANROADS), Ofisi ya Waziri Mkuu– TAMISEMI,
TARURA na Mfuko wa Barabara (Road Fund).


.jpeg)
0 Maoni