Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Wilaya ya Kibiti ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Bungu, Mhe. Ramadhan Mpendu,
ameongoza zoezi la upandaji miti katika Shule ya Sekondari Nyambili–Nyambunda
jana, ikiwa ni sehemu ya kampeni endelevu ya kutunza mazingira.
Katika zoezi hilo, jumla ya
miti 150 ya matunda na kivuli imepandwa shuleni hapo, ambapo Mhe. Mpendu
aliipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa uzalishaji na
usambazaji wa miche bure kwa wananchi na taasisi mbalimbali.
“Tutunze miti, itatufaa kwa
vizazi vijavyo. TFS wamefanya kazi kubwa – miche hii ni dira ya mustakabali wa
mazingira bora,” alisema Mhe. Mpendu mara baada ya zoezi hilo kukamilika.
Viongozi wengine
waliohudhuria ni pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Mhe. Omari
Msumi, Mkuu wa shule ya Sekondari Nyambili–Nyambunda, walimu pamoja na
wanafunzi wa shule hiyo ambao walishiriki kikamilifu katika upandaji miti.
Mhe. Mpendu pia aliwatia
moyo walimu na wanafunzi kwa kujitoa kwao katika kutunza mazingira, akisema
shule hiyo inatoa mfano bora wa kuigwa katika kulinda
rasilimali za asili.
0 Maoni