Tanzania kuzuia mazao kutoka Malawi na Afrika Kusini

 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo itazuia uingizwaji wa mazao na bidhaa zote za kilimo kutoka nchi za Malawi na Afrika Kusini ifikapo Jumatano ya wiki ijayo, iwapo mataifa hayo mawili hayataondoa zuio la mazao ya kilimo kutoka Tanzania.

Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Kilimo Mh. Hussein Bashe imesema kwamba Serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kufungua soko mazao ya kilimo ya Tanzania kwa nchi za Malawi pamoja na soko la ndizi nchini Afrika Kusini bila mafanikio.

“Serikali imepokea taarifa rasmi kuwa Serikali ya Malawi imezuia kuingia kwa mazao ya kilimo kutoka Tanzania, yakiwemo unga, mchele, tangawizi, ndizi, na mahindi. Hatua hii imeathiri moja kwa moja shughuli za wafanyabiashara wetu wanaosafirisha bidhaa hizo kwenda Malawi,” amesema Mh. Bashe.

Mh. Bashe ameeleza pia, kwa kipindi cha miaka mitano, Serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kufungua soko la ndizi nchini Afrika Kusini bila mafanikio. “Hali hii inafanana na changamoto tulizopitia kwa zaidi ya miaka kumi katika kufungua soko la parachichi, hadi pale tulipoamua kuchukua hatua za kulinda maslahi ya nchi yetu.”

“Iwapo Serikali ya Malawi na Afrika Kusini hazitabadilisha msimamo wao kufikia Jumatano ijayo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo itazuia uingizwaji wa mazao na bidhaa zote za kilimo kutoka nchi hizo mbili,” amesema Mh. Bashe.

Amesema kwamba bidhaa za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini haitaruhusiwa kupita ndani ya mipaka ya Tanzania, kuelekea bandari ya Dar es Salaam au nchi nyingine yoyote, hadi zuio hilo litakapoondolewa.

Pamoja na mambo mengine Mhe. Bashe  amesema usafirishaji wa mbolea kwenda Malawi utasitishwa, ikiwa ni sehemu ya hatua za kulinda maslahi ya wakulima na wafanyabiashara wa Kitanzania.

“Wasafirishaji wote wa Kitanzania wanaosafirisha bidhaa za kilimo, ninawashauri kuacha kupakia bidhaa hizo mpaka hapo Malawi na Afrika Kusini watakapo badilisha msimamo wao,” ameshauri Mhe Bash na kuongeza,

“Wafanyabiashara walioweka order za apples, machungwa, na bidhaa zingine ambazo hununuliwa Afrika kusini, ninawashauri kuacha kwa sasa kwani hatutoziruhusu kuingia Tanzania mpaka hapo Afrika Kusini itakapo tufungulia soko la ndizi.”

Hatua hizi ni za kulinda heshima ya nchi yetu, uchumi wa wakulima wetu, na usawa katika biashara za kikanda, imemelizia taarifa hiyo ya  Mh. Hussein Bashe- Waziri Wa Kilimo Tanzania.

Chapisha Maoni

0 Maoni