Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameupongeza uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bukombe kwa Mkutano Mkuu Maalum wa kutoa taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM Jimbo la Bukombe kwa mwaka 2020-2025.
Rais Mstaafu
Kikwete ametoa pongezi hizo leo Februari 8, 2025 wakati akihutubia katika
Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliofanyika katika Kata ya Igulwa, Wilaya ya
Bukombe, Mkoa wa Geita.
“ Nawapongeza
kwa kuandaa Mkutano huo kwa kuwa unakidhi takwa la katiba ya CCM kwa kuwa
inawezesha kupima mlipotoka, mlipo na mnapokwenda. Katiba ya Chama Cha
Mapinduzi ya mwaka 1977 toleo la 2022 katika Ibara ya 72 (1) inatambua kuwa
Mkutano Mkuu ni kikao kikubwa cha Chama katika ngazi ya wilaya, aidha Ibara ya
74 imetamka kazi za msingi za Mkutano huu kuwa ni kuzungumza mambo yote
yanayohusu ulinzi na usalama na maendeleo kwa ujumla katika wilaya,” amesema
Rais Mstaafu Kikwete.
Ameendelea
kwa kuwasihi wanachama wa CCM kudumisha umoja na mshikamano “ Wekeni mbele
maslahi ya Chama chetu, watajitokeza watu mbalimbali kuja kugombea nafasi
mbalimbali wapokeeni lakini wakitokea wenye maneno tu waambieni sie tunataka
maendeleo sio maneno"
Akizungumzia
utekelezaji wa Ilani ya CCM Bukombe amempongeza Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kutoa fedha nyingi zilizosaidia utekelezaji wa idadi kubwa ya miradi
ya maendeleo katika Jimbo hilo.
“Nyie wenyewe
mmeona yaliyofanyika Bukombe ni mengi sana na hakuna mkoa wilaya au jimbo
ambalo halikuguswa na Rais Samia. Hii ndio sababu ya msingi iliyofanya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum
uliofanyika Dodoma Januari mwaka huu
kumchagua kuwa mgombea wa chama chetu kwa nafasi ya urais katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025,” amesema Rais Mstaafu Kikwete.
Amebainisha
kuwa miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa inaonekana na ina faida
kwa wananchi huku akieleza jitihada za Dkt. Biteko za kuleta maendeleo katika
Jimbo hilo. “ Naomba kuwahakikishia kuwa hamkufanya makosa kumpa kura zenu Dkt.
Biteko, naomba niwaambie kuwa mambo haya mazuri ya Bukombe yasingetokea
kama msingemchagua Dkt. Biteko.”
Aidha, Rais
Mstaafu Kikwete amewaasa wananchi wa Bukombe kuwachagua wagombea wa CCM katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ili kuendeleza miradi ya maendeleo katika Jimbo
hilo.
Katika hatua
nyingine, Rais Mstaafu Kikwete amemshukuru na kumpongeza Rais Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa uongozi wake mzuri wa nchi na kuwa nchi imetulia na ina amani
na maendeleo yanaonekana katika kila eneo.
Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt.
Doto Biteko wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi Bukombe kwa mwaka 2020 - 2025 amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo jimboni humo.
“ Nianze kwa
kusema kwa yote yaliyotekelezwa katika Jimbo hili yametokea kwa sababu ya matashi mema ya Rais wetu Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatupenda
sana wananchi wa Bukombe, kwa kipindi ambacho nimekuwa mbunge
nimeona ametoa fedha nyingi sana kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya
Jimbo leo,” amesema Dkt. Biteko.
Vilevile,
amesema kuwa Rais Samia ameridhia ujenzi wa barabara ya kutoka Ushirombo hadi
Katoro kwa kiwango cha lami na kuwa mkandarasi anatafutwa kwa ajili ya kuanza
ujenzi.
Ameongeza
kuwa Wilaya ya Bukombe inatarajia kutekeleza mradi mkubwa wa nishati ya umeme
katika Kata ya Busonzo ambao utazalisha megawati 5 zitakazoingizwa katika gridi
ya Taifa.
Awali
akiwasilisha taarifa ya miradi ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya
CCM kwa njia ya makala ya picha jongefu,
Dkt. Biteko ametaja miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa
miundombinu, huduma za afya, maji, usambazaji wa nishati, ujenzi wa madarasa,
mabweni, maabara na matundu ya vyoo katika shule za msingi na sekondari.
Katika sekta
ya nishati, makala hiyo inaeleza kuwa huduma ya usambazaji umeme imefika katika
vijiji vyote 64 vya Jimbo hilo ili kuendelea kukuza fursa za uwekezaji na
kukuza uchumi kwa wananchi.
Katika sekta
ya elimu, sehemu ya makala hiyo inataja miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa
nyumba ya mwalimu katika Shule ya Msingi Bulumbaga wenye gharama ya Sh.
40,000,000.00; ujenzi wa vyumba nane vya madarasa katika Shule ya Sekondari ya
Msonga- Ikuzi (Mpya) wenye gharama ya Sh. 160,000,000.00 na ujenzi wa matundu
ya vyoo ishirini na nane katika shule ya msingi Msonga wenye gharama ya
shilingi milioni 47,439,000,00.
Aidha, katika
sekta ya afya, ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na uboreshaji wa hospitali ya
wilaya umesaidia kuboresha huduma za afya katika hospitali na kuboresha hali za afya za wananchi kupitia
miradi mbalimbali ikiwemo ukamilishaji wa Zahanati ya Kagwe kwa gharama ya Sh.
50,000,000.00., ukamilishaji wa Zahanati ya Lyambomgongo kwa gharama ya Sh.
50,000,000.00 na ujenzi wa Zahanati ya Ishololo kwa gharama ya Sh.
101,223,889.86.
Aidha, miradi
mingine iliyotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao ya
kilimo Msangila kwa gharama ya Sh.
993,314,906.24, uchimbaji wa kisima kirefu katika kijiji cha Namonge Sh.16,
348,900.00 na matengenezo ya sehemu korofi katika barabara ya Uyovu - Namonge –
Namarandula (1.50Km) kwa gharama ya Sh. 90,161,000.00.
Sambamba na
hayo, Dkt. Biteko amewashukuru madiwani wote wa Jimbo lake kwa kusimamia vizuri
miradi ya maendeleo katika maeneo yao huku akiwahakikishia kuendelea
kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali zinazolenga kuboresha maisha ya
wananchi wao.
Mkuu wa Mkoa
wa Geita, Mhe. Martin Shigella amempongeza Rais Mstaafu Kikwete kwa jitihada alizofanya wakati wa uongozi wake
kwa kujenga msingi mzuri wa kuhakikisha watoto wanapata elimu nchini.
“ Katika
uongozi wa Rais Samia tumejenga shule mpya 150 na wakati ule unatengeneza Ilani Mhe. Rais Mstaafu
Kikwete uliona mzigo kwa wazazi kusomesha watoto na sasa katika uongozi wa Rais
Samia kila mwezi tutapokea shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya kusomesha watoto,” amesema Mkuu wa Mkoa Shigella.
Ameongeza “ Rais Samia ametuleta magari 15 ya kubeba wagonjwa mahututi ambayo
tumeyagawa katika hospitali zetu na vituo vya afya. Mkoa wetu pia umepata zaidi
ya dola milioni 165 zitakazosaidia kupeleka maji Chato, Wilaya ya Geita na vijijini, hivyo
kufikia malengo ya Serikali ya kufikisha huduma ya maji safi na salama kwa
jamii.
Mwenyekiti wa
Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Bukombe, Matondo Luhonja amesema kuwa Mbunge wa
Bukombe, Dkt. Biteko amekuwa kiongozi msikivu, makini na mwenye ushirikiano na
wananchi wake na hivyo mafanikio hayo ya utekelezaji yamechangiwa pia na uongozi wake mzuri.
Mkutano huo
Mkuu wa CCM Bukombe umehudhuriwa na maelfu ya wananchi wa Bukombe uliambatana
na burudani kutoka kwa msanii wa muziki wa kizazi kipya Harmonize.
Na. Ofisi ya
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni