RAIS Mstaafu Dk.Jakaya Kikwete ameamua kuwatolea
uvivu wale ambao wamekuwa wakimzushia kifo ambapo amesema yeye ni mzima wa afya
hana mafua wala kichomi na kusisitiza wanaomuombea mabaya watatangulia wao na
atahudhuria mazishi yao.
Mzee Kikwete ambaye ni Rais Mstaafu was Serikali ya
Awamu ya Nne ameyasema hayo leo Oktoba 10,2025 alipokuwa akiwasalimia wakazi wa Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani,
katika Mkutano wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) ulioongozwa na Mgombea
Mwenza wa Urais kupitia CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi.
“Wale
wanaonizushia kifo kupitia
mitandao ya kijamii niwaambie niko salama, afya yangu ni nzuri,sina
mafua wala kichomi,wanaomwombea mabaya watatangulia wao na mimi
nitahudhuria mazishi yao.”
Kikwete ametoa kauli hiyo baada ya kueleza sababu
zinazowafanya wananchi kukiamini Chama
Cha Mapinduzi kutokana na mikakati na uwezo wa chama hicho katika kupangilia
mambo.
Amesema uwezo huo ndio unasababisha CCM kuendelea
kuongoza Serikali, na pale anaposema CCM itaendelea kuongoza nchi, wanainuka
watu wengine wasiopenda kauli hiyo na kumzushia kifo.
Pamoja na hayo, Kikwete ametumia fursa hiyo pia
kumwombea kura Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM,
Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mgombea Mwenza Dkt. Emmanuel Nchimbi, na wagombea
wengine wa Bagamoyo.



0 Maoni