Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM),
Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito mzito kwa Watanzania kutumia hekima na
busara zao wanapojiandaa kuchagua viongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao. Dkt.
Samia amesisitiza kuwa uongozi wa nchi unahitaji uzoefu, uthubutu na weledi na
haupaswi kupewa kwa mtu yeyote kama eneo la majaribio.
Akizungumza
katika mkutano mkubwa wa hadhara mjini Bunda, Mkoa wa Mara, Rais Samia
alikumbusha umuhimu wa kura kama dhamana ya Taifa. "Kabla hujafanya
maamuzi, fikiria kwanza," alisisitiza Dkt. Samia. "Nchi si darasa la
majaribio; mpe mamlaka yule unayemwamini ataiongoza kwa hekima na kuhakikisha
maslahi ya Watanzania yanalindwa."
Rais
alibainisha kwamba kipindi hiki si cha kurudi nyuma au kuanza upya, bali ni cha
kuendeleza kasi ya maendeleo iliyopatikana. Alisema Serikali inayoongozwa na
CCM imejenga msingi imara katika sekta zote muhimu, ikiwemo elimu, afya,
miundombinu, na nishati.
"Tumejenga
msingi imara. Tunahitaji kuilinda kasi hiyo kwa kufanya maamuzi sahihi. Kura
zetu ndizo nguzo pekee ya kuendeleza amani, umoja, na mafanikio ya taifa
hili," alisema Rais huku akishangiliwa na umati wa wananchi wa Bunda.
Aliongeza kuwa maendeleo yanayotarajiwa ni matokeo ya uamuzi makini utakaofanywa
na kila mpiga kura.
Ziara ya Dkt.
Samia, ambayo inaendelea kunadi Ilani ya CCM ya 2025–2030, inalenga
kuwashirikisha wananchi katika safari ya kujenga Tanzania yenye ustawi wa
kiuchumi na kijamii.
Rais Samia
alisisitiza kwamba Watanzania wanajua thamani ya utulivu na maendeleo. Kura si
tu kitendo cha kidemokrasia, bali ni sauti ya uamuzi makini, sauti ya busara,
na sauti ya Tanzania yenye matumaini. Alihitimisha kwa kuwahimiza wananchi
kuhakikisha wanatoa kura zao kwa chama pekee kinachoweka maslahi ya wananchi
mbele, akisisitiza kuwa chama hicho ni CCM.

0 Maoni