WAZIRI MKUU,
Kassim Majaliwa amesema mfumo wa anwani za makazi utasaidia kuchochea ukuaji wa
uchumi, kuharakisha upatikanaji wa huduma za kijamii, kuimarisha masuala ya
ulinzi na usalama, kuwezesha biashara mtandao kufanyika kwa ufanisi na
kuimarisha uwezo wa kukabiliana na majanga.
Ameyasema
hayo leo (Jumamosi, Februari 8, 2025) katika maadhimisho ya kilele cha Wiki ya
Anwani za Makazi yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete,
jijini Dodoma. Katika kilele hicho Waziri Mkuu amezindua matumizi ya mfumo wa
Anwani za Makazi. Kaulimbiu za maadhimisho hayo inasema “tambua na tumia anwani
za makazi kurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma”.
Waziri Mkuu
amesema suala la anwani za makazi ni moja ya masuala yaliyopewa kipaumbele
katika Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo wa Taifa 2021/2022- 2025/2026 ambao
umeweka bayana azma ya Serikali ya kujenga mfumo wa anwani za makazi na
postikodi katika kata zote nchini.
“...siku kama
ya leo tarehe 8 Februari, 2022, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,
alizindua utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi nchini kwa njia ya operesheni.
Operesheni hiyo ilifanyika kwa muda wa miezi minne na kuwezesha ukusanyaji wa
taarifa milioni 12.3 za anwani za makazi zilizohifadhiwa katika mfumo wa
kidijitali wa anwani za makazi unaojulikana kwa jina la National Physical
Addressing (NaPA).
Amesema
kupitia programu ya NaPA mwananchi akiwa eneo lolote nchini na hujui sehemu ya
kupata huduma za kijamii kama vile kituo cha afya au mgahawa anaweza kutumia
programu hiyo kutafuta sehemu za karibu. “Hii ni programu bora na inarahisisha
kupata huduma husika sambamba na kwenda na kasi ya kimaendeleo katika uchumi wa
sasa wa Kijiditali.”
Pia, Waziri
Mkuu amewasisitiza wananchi kutunza na kuwa walinzi wa miundombini ya anwani za
makazi kwa kuwa Serikali imetumia gharama kubwa katika kugharamia miradi hiyo.
“Vibao tulivyoviweka kuonesha mitaa na barabara, tunao Watanzania ambao si
waaminifu wanang’oa mabago hayo na kwenda kuyauza, ni muhimu kila mmoja kuwa
mlinzi wa miundombinu hiyo kwa sababu inamanufaa.”
Kwa upande
wake, Waziri Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema Wizara ya
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaendelea kusimamia na kuendeleza
miundombinu na mifumo ya msingi (Foundation Systems), ambayo ni mhimili muhimu
wa uchumi wa kidijitali ulioainishwa katika Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa
Miaka 10 (2024–2034).
Amesema
mifumo hiyo inajumuisha mifumo ya utambuzi wa watu, biashara, ardhi, na makazi.
“Katika muktadha huu, utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi ni hatua ya
kimapinduzi inayolenga kuboresha utambuzi na utoaji wa huduma kwa wananchi hapa
nchini.”
Naye, Naibu
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Nadir Abdulatiff Awady amesema zoezi la uwekaji wa anwani za makazi kwa upande
wa Zanzibar limekamilika kwa asilimia 100, ambapo kwa sasa wanaendelea
kuwahamasisha wananchi matumizi ya anwani hizo.
Awali, Naibu
wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt, Festo Dugange alisema kabla ya
utekelezaji wa mfumo huo ilikuwa ni vigumu kwa mgeni kufika katika baadhi ya
maeneo ila kwa sasa imerahisishwa baada ya
utekelezwaji wa mpango huo.
0 Maoni