Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonesha wasiwasi mkubwa
kuhusu athari za kusitishwa mara moja kwa ufadhili wa programu za HIV katika
nchi za kipato cha chini na cha kati.
Programu hizi hutoa ufikiaji wa tiba ya kuokoa maisha ya HIV
kwa zaidi ya watu milioni 30 duniani. Takwimu za WHO zinaonyesha watu milioni
39.9 walikuwa wakiishi na virusi vya HIV mwishoni mwa 2023.
Kusitishwa kwa ufadhili wa programu za HIV kunaweza kuwaweka watu wanaoishi na virusi vya HIV katika hatari ya magonjwa na kifo na kudhoofisha juhudi za kuzuia maambukizi katika jamii na nchi.
Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na
UKIMWI (PEPFAR), umekuwa mpango mkuu wa mwitikio wa HIV duniani tangu
kuanzishwa kwake zaidi ya miaka 20 iliyopita.
WHO imesema kusitishwa kwa sasa kwa ufadhili wa PEPFAR
kutakuwa na athari ya moja kwa moja kwa mamilioni ya maisha ambayo yanategemea
usambazaji wa matibabu salama na madhubuti ya kurefusha maisha.
PEPFAR inafanya kazi katika nchi zaidi ya 50 duniani kote.
Katika miongo miwili iliyopita, ufadhili wa PEPFAR umeokoa maisha ya zaidi ya
milioni 26.
Kwa sasa, PEPFAR inatoa matibabu ya HIV kwa zaidi ya watu milioni 20 wanaoishi na virusi vya HIV duniani kote, wakiwemo watoto 566,000 walio chini ya umri wa miaka 15.
0 Maoni