Wananchi wa Kata ya Mgama, wilaya ya Iringa, wameeleza
furaha yao kutokana na maendeleo makubwa ya ujenzi wa barabara ya Wenda-Mgama,
ambayo kwa sasa imefikia asilimia 90 ya utekelezaji.
Barabara hiyo, yenye urefu wa kilomita 19, inajengwa kwa
kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi bilioni 29.7 chini ya mradi wa RISE,
unaofadhiliwa na mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia.
Mradi huo unalenga kurahisisha usafirishaji wa mazao ya
misitu, mbogamboga, chai, na mazao mengine kutoka mashambani hadi sokoni kwa wakati.
Wananchi wameeleza matumaini makubwa ya kuboreka kwa maisha
yao kutokana na faida ya barabara hiyo.
Akizungumza wakati wa ziara ya Mtendaji Mkuu wa Wakala ya
Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff, mkazi wa eneo
hilo Bi. Leah Mhelela amesema, “tulikuwa tunahangaika sana hasa wakati wa mvua.
Sasa hivi tunaona mwanga wa matumaini kwa sababu mazao yetu yatafika sokoni kwa
wakati na bila kuharibika.”
Naye, Witelini Mbata
amesema barabara hiyo itapunguza gharama za usafirishaji na muda wa
safari. “tulikuwa tunatumia muda mwingi barabarani kwa sababu ya ubovu wa
barabara. Sasa tuna hakika, kwamba hali itabadilika na kazi yetu itakuwa rahisi
zaidi," alisema kwa furaha.
Mhandisi Mshauri wa mradi huo, Edga Laurian, ameeleza kuwa
mradi umefikia asilimia 90 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Februari
mwaka huu.
Barabara ya Wenda-Mgama ina umuhimu mkubwa kiuchumi na
kijamii, kwani inaunganisha vijiji mbalimbali na maeneo ya biashara. Kukamilika
kwake kutasaidia pia kuboresha huduma za kijamii, kama usafiri kwa wagonjwa na
wanafunzi, na hivyo kuongeza maendeleo katika eneo hilo.
Wananchi wana matumaini makubwa kuwa barabara hiyo itafungua fursa nyingi za kiuchumi na kuboresha maisha yao kwa ujumla.
0 Maoni