Foleni ya kupata mafuta badala ya foleni ya kupiga kura
ndiyo hofu inayowatawala wananchi wa Malawi wengi mawazoni mwao huku uchaguzi
mkuu wa nchi hiyo utaofanyika Jumanne ukikaribia.
Upungufu wa mafuta wa muda mrefu, pamoja na kukatika kwa
umeme mara kwa mara, kupanda kwa gharama za maisha, njaa, umasikini, ukosefu wa
usawa na ukosefu wa ajira kwa vijana, vinaongeza hasira na hali ya kukata tamaa
inayoonekana wazi hapa.
Wagombea wa urais, ubunge na halmashauri za mitaa wanashindana
kutafuta kura katika mazingira ya kutoaminika kuhusu ni nini hasa kinaweza
kubadilika.
Katika ishara kwamba hali ya kifedha ni ngumu, kampeni za
uchaguzi zimekuwa za kimya zaidi ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Hii ni licha ya uchaguzi wa urais kuonekana kama marudio ya
mchuano kati ya rais wa sasa, Lazarus Chakwera, na mtu aliyemshinda mwaka 2020,
ambaye alikuwa Rais wakati huo, Peter Mutharika. Kuna wagombea wengine 15 pia.
Matamasha ya kampeni yenye rangi na shamrashamra za kawaida hayapo. Fulana za bure ambazo kwa kawaida hugawiwa kwa wingi ili kuchochea hamasa, mwaka huu zimetolewa kwa kiwango kidogo zaidi.
0 Maoni