Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wa
Taifa wa chama, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema, akichaguliwa kuwa rais
katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, serikali atakayoiongoza itaufanya Mkoa wa Kigoma
kuwa kitovu cha biashara katika Ziwa Tanganyika na nchi zinazouzunguka mkoa
huo.
Dkt. Samia ametoa kauli hiyo Jumamosi Septemba 13, 2025
alipohutubia mikutano ya kampeni katika wilaya za Uvinza, Kasulu na Buhigwe
mkoani Kigoma.
Amesema mkoa huo una fursa nyingi na tayari serikali yake
imefanya mambo makubwa ambayo yameufungua kiuchumi.
Ameyataja mambo ambayo serikali yake itayafanya akichaguliwa
Oktoba 29,2025 ni pamoja na kufua umeme wa megawati 49.5 katika mto Malagarasi zinazokwenda
kuongeza nguvu ya nishati hiyo kwa mkoa huo.
Alisema kutokana na masafa marefu ya kusafirisha umeme
kufika Kigoma, kumekuwa na changamoto kiasi, hivyo umeme wa Malagarasi unaenda
kuwa jawabu la changamoto hiyo.
Aidha, alisema umeme huo mwingi utaenda kuvutia uwekezaji
zaidi wa viwanda vilivyopo na vile vitakavyokuwa katika kongani za wilaya za
mkoa wa Kigoma.
Aliitaja hatua nyingine itakayoifanya Kigoma kuwa kitovu cha
biashara ni ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambayo alieleza mkoa huo utakuwa na
vituo vingi kuliko mkoa mwingine.
"Hii reli ya SGR itakuwa ni fursa nyingine kwa Kigoma, kwanza Kigoma itakuwa ndio mkoa wenye vituo vingi vya SGR. Na itafungua fursa nyingi za kibiashara ndani na nje ya nchi na kuifanya Kigoma kuwa kitovu cha biashara," alisema Dkt. Samia katika mkutano wake uliofanyika kwenye Uwanja wa Kiganamo, Kasulu Mjini.
Pia alisema kuwa kutajengwa maghala kwa ajili ya kuhifadhi bidhaa.
Dkt. Samia alisema tayari kuna viwanda vya sukari na saruji mkoani humo ambavyo ni vya kimkakati, na cha sukari kimeshatoa ajira 500 kwa vijana wa Kasulu.
Ujenzi wa meli na ukarabati wa Mv Ilagala na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma ni eneo jingine aliloeleza kuwa linaenda kubadili ustawi wa maisha ya watu wa mkoa huo.
Kuhusu kilimo, amesema mkoa huo unazalishaji kwa wingi mazao mbalimbali hivyo akawataka wakulima wauze mazao yao nje lakini wasisahau kujiwekea akiba ya chakula.
Aliwataka wana CCM na wananchi kwa ujumla wachague wagombea wote wa CCM katika ngazi zote kwa sababu serikali atakayoingoza akipewa ridhaa na watanzania, imedhamiria kuwainua watu wa hali ya chini, badala ya vyama vinavyohubiri masuala ya 'kukiwasha'.
Jumapili Septemba 14 mgombea huyo wa CCM atahitimisha mikutano yake ya kampeni mkoani Kigoma kwa mkutano mkubwa utakaofanyika Kigoma Mjini.
Na. Aboubakary Liongo - Mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM
0 Maoni