Ujenzi wa Kituo cha Afya Mahonda wafikia mwisho, kufunguliwa Januari

 

Wizara ya Afya Zanzibar imesema ujenzi wa Kituo cha Afya Mahonda umekamilika kwa asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Januari mwakani, ambapo utafunguliwa rasmi wakati wa sherehe za Mapinduzi.

Akizungumza wakati wa ziara maalumu ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo, Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema kituo hicho kitakuwa kinatoa huduma mbalimbali za afya zikiwemo huduma za kliniki za nje, uzazi, chanjo na huduma nyingine muhimu kwa jamii.

“Tumefikia hatua nzuri. Tunatarajia kituo hiki kitafunguliwa Januari mwakani na tunawataka wakandarasi kuongeza kasi ili wananchi waanze kunufaika na huduma bora,” alisema Waziri Mazrui.

Ameeleza kuwa kazi inayoendelea inaonekana kufanyika kwa viwango vya kuridhisha na matarajio ya Serikali ni kuona mradi huo unamalizika kwa ubora uliokusudiwa.

Kwa upande wake, mkandarasi anayejenga kituo hicho, Juma Yussuf Hashim, alisema ujenzi ulianza Desemba mwaka jana na umepangwa kukamilika Januari 2026 kama ilivyopangwa.

“Tumejipanga kuhakikisha tunamaliza kazi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa. Mpaka sasa kazi inaenda vizuri,” alisema mkandarasi huyo.

Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Mahonda unafadhiliwa na Serikali ya Oman na unahusisha majengo matano, yakiwemo majengo ya Block A, B na C.

Katika ziara hiyo, Waziri Mazrui pia alitembelea Kituo cha Afya Kinduni na nyumba za madaktari zilizopo Hospitali ya Wilaya ya Pangatupu.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo alipokea msaada wa miwani 500 kutoka kwa mfanyabiashara Said Salim Bopar, ambazo zitagawiwa kwa watu wenye matatizo ya macho, wakiwemo watoto.

“Nusu ya miwani hizi ni kwa ajili ya watoto wenye matatizo ya macho, ili kuwasaidia kuendelea vizuri na masomo yao,” alisema Waziri Mazrui.

Alimshukuru mfanyabiashara huyo kwa kuendelea kuisaidia sekta ya afya, akitaja misaada mingine aliyowahi kutoa kama vitanda na magodoro kwa ajili ya wagonjwa.

“Tunashukuru kwa msaada huu. Ni ishara ya mshikamano kati ya sekta binafsi na Serikali katika kuboresha huduma za afya,” aliongeza.



Chapisha Maoni

0 Maoni