Wanafunzi
watatu walijeruhiwa Jumanne baada ya ndege ndogo isiyo na rubani ya Jeshi la
Ulinzi la Rwanda (RDF) kuanguka katika Wilaya ya Rutsiro, magharibi mwa Rwanda,
kufuatia kupoteza mwelekeo wakati wa mazoezi ya kijeshi kutokana na hali mbaya
ya hewa.
Kwa
mujibu wa taarifa ya RDF, ndege nyuki hiyo ya kijeshi ilipoteza mwelekeo majira
ya saa 7:40 mchana na ikaanguka katika eneo la makazi wakati wanafunzi
wakirejea nyumbani kutoka shuleni.
Wanafunzi
wawili kati ya watatu waliopata majeraha wanapatiwa matibabu katika Kituo cha
Afya cha Kivumu, huku mmoja akihamishiwa katika Hospitali ya Murunda kwa
matibabu ya kina.
Katika
taarifa yake kwa umma, RDF ilieleza kuwa inaungana na familia za watoto
walioumia kwa huzuni na kuahidi kugharamia kikamilifu matibabu yao.
Maafisa
wa jeshi wamesema wanaendelea kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa
pamoja na wataalamu wa afya ili kuhakikisha watoto wote walioathirika wanapata
huduma bora za kitabibu.
"Hili
ni tukio la kusikitisha, na tutatoa msaada wote unaohitajika kwa watoto
walioumia pamoja na familia zao," ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo ya RDF.
0 Maoni