Townsend aomba radhi kwa kuviponda vyakula vya kichina

 

Mchezaji nyota wa tenisi kutoka Marekani, Taylor Townsend, ameomba radhi kufuatia kauli zake za kuviponda vyakula vya jadi vya Kichina alizotoa kupitia mitandao ya kijamii, ambazo zimeibua mjadala mkali.

Townsend (29), ambaye kwa sasa yuko katika jiji la Shenzhen nchini China kwa ajili ya mashindano ya Billie Jean King Cup Finals, alichapisha video kupitia Instagram akizungumzia baadhi ya vyakula alivyovikuta, ikiwemo vyenye vyura, kasa na tango bahari, akisema:

“Hii ni kitu cha ajabu kabisa kuwahi kuona... Inabidi niongee na HR... kula kasa na vyura ni kitu cha mwituni sana.”

Kauli hiyo ilisababisha mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii, si tu kwa Kiingereza bali pia kwenye majukwaa ya Kichina, ambako wengi walieleza kuchukizwa na namna alivyodhalilisha utamaduni wa chakula wa China.

Baadaye, Townsend ambaye kwa sasa ndiye mchezaji namba moja kwa ubora duniani upande wa mchezo wa ‘doubles’, aliomba radhi akisema:

“Hakuna kisingizio, sina maneno… kwangu mimi, nitajirekebisha na kuwa bora zaidi.”

Kauli hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti, huku wengi wakisisitiza umuhimu wa kuheshimu tamaduni za wenyeji, hasa kwa watu maarufu wanaotembelea mataifa ya wengine.

Chapisha Maoni

0 Maoni