Mamlaka
ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii
kwa kushirikiana na Idara ya Huduma za Uhandisi, inaendelea na jitihada za
kuimarisha miundombinu ya maji katika vijiji vya Sendui na Irkeepusi, vilivyopo
Tarafa ya Ngorongoro, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuboresha upatikanaji wa
huduma hiyo muhimu kwa wanyamapori, mifugo na wakazi wa maeneo hayo.
Tathmini
iliyofanywa na wataalamu wa mamlaka hiyo imeainisha maeneo yenye uhitaji wa
maboresho, ikiwemo ukarabati wa birika la kunyweshea mifugo katika kijiji cha
Sendui, ambalo kwa sasa linahudumia pia vijiji vya jirani vya Alailelai na
Bulati.
Aidha,
ukaguzi umefanyika katika mradi wa ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita
140,000 lililopo katika Shule ya Sekondari ya Nainokanoka. Tanki hilo limekuwa
msaada mkubwa kwa wanafunzi wa shule hiyo pamoja na wakazi wa kijiji cha
Irkeepusi na maeneo jirani.
Kwa
mujibu wa taarifa ya wataalamu hao, tanki hilo linalenga kuhudumia pia Shule ya
Msingi Irkeepusi, lango la Lemala (Lemala Gate) na hoteli mbalimbali zilizopo
katika eneo hilo.
Mbali na
uboreshaji wa miundombinu, wataalamu wa NCAA kwa kushirikiana na viongozi wa
jamii wamekuwa wakitoa elimu ya utunzaji wa vyanzo na miundombinu ya maji kwa
wananchi, ili kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu na inaleta manufaa kwa
muda mrefu.
Mamlaka
ya Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ikitekeleza miradi ya kijamii kama sehemu ya
juhudi za kuhakikisha uhifadhi shirikishi, unaowezesha wananchi kunufaika moja
kwa moja na rasilimali zilizopo katika eneo hilo la urithi wa dunia.
0 Maoni