Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imefanikiwa
kumpandikiza figo (kwa mafanikio) Mgonjwa wa Hamsini (50) tangu kuanzishwa kwa
huduma ya upandikizaji figo Hospitalini hapo tarehe 22 Machi, 2018.
Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi amesema kuwa
Mgonjwa huyo Emmanuel Woiso (38) ambaye leo ameruhusiwa kurudi nyumbani
kuendelea na shughuli zake ni mafanikio makubwa katika huduma za kibingwa
bobezi ambazo zinatolewa na Wataalamu Wazawa na amempongeza Mhe Rais Samia
Suluhu Hassan kwa kuendeleza uwekezaji Mkubwa anaoufanya katika Sekta ya Afya
inayowezesha huduma kama hizi kupatikana hapa nchini ambapo hapo awali zilikuwa
zikipatikana nje ya nchi tu.
“Takribani miaka 6 iliyopita Hospitali ya Benjamin Mkapa
ilikuwa kituo cha pili hapa nchini kuanza kutoa huduma hiyo ambapo kati ya
Wagonjwa hao 50 waliopandikizwa hapa BMH, asilimia 95% wanaishi na kuendelea na
majukumu yao,” alisisitiza Prof. Makubi.
Ameongeza kuwa takribani asilimia 98% ya Wagonjwa
wanaopandikizwa figo wanaendelea kuishi na kufanya majukumu yao baada ya
kipindi cha mwaka mmoja tangu kupata huduma hiyo huku wastani wa asilimia 86%
wakiendelea kuwa hai baada ya miaka mitano tangu kupata huduma jambo
linaloonesha ubora wa huduma hii hapa nchini kuwa ni mzuri kwa viwango
vinavyofanana na maeneo mengine Duniani kama Marekani, Ulaya na India.
Akizungumzia gharama za matibabu hayo Prof. Makubi
amesema kuwa kwa sasa Serikali inaingia gharama ya wastani wa Shilingi 34
Milioni kumtibu Mgonjwa wa figo hapa nchini ukilinganisha na Wastani wa
Shilingi 64 Milioni kumtibu Mgonjwa nje ya nchi kama India na Ulaya, hivyo kwa
Wananchi hao 50 waliotibiwa figo hapa BMH Serikali imetumia takribani Shilingi
1.7 Bilioni ikilinganishwa na takribani Shilingi 3.3 Bilioni endapo wananchi
hao wangetibiwa nje ya nchi hivyo kuokoa takribani shilingi 1.6 Bilioni.
Prof. Makubi amesema mwelekeo wa BMH katika mwaka 2025 ni
kuongeza zaidi kasi ya huduma za upandikizaji figo kwa kutumia teknolojia za
kisasa zaidi za upasuaji uvunaji figo wa matundu madogo (Laparoscopic
Nephrectomy) badala ya kupasua sehemu kubwa ya mwili katika kuvuna figo na pia
kuwekeza katika upasuaji wa kutumia Robot (Robotic Surgery) ambazo hurahisisha
kazi kwa watalaamu.
“Tuna kituo chetu cha matibabu ya figo tunakwenda
kukipanua kiwe kituo cha umahiri cha upandikizaji wa figo hapa nchini na Afrika
Mashariki na Kati kwa ufadhili wa Serikali ya Japan kwa gharama ya takribani
Shilingi 33 Bilioni ambapo tunashirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo
tutabobea katika Robotic Surgeries,” alimalizia Prof. Makubi.
Naye Bw. Emmanuel Woiso ambaye amepata huduma ya matibabu
ya kupandikizwa figo hapo BMH, amesema kuwa ametembea kwenye Hospitali kadhaa
kubwa hapa nchini na kushauriwa afike BMH ndipo ataweza kupata matibabu hayo ya
kupandikizwa figo.
“Baada ya kufika BMH nikaanza kuchukuliwa vipimo na baada
ya Vipimo kwenda vizuri nikapangiwa uperesheni ya kupandikizwa figo na baada ya
matibabu hayo kukamilika hali yangu sasa najiskia vizuri, naishukuru Serikali
kwa kuboresha huduma hizi za Afya na kutuwezesha sisi Wananchi kuzipata
hapahapa nchini,” alishukuru Bw. Emmanuel Woiso.
0 Maoni