Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba amesema zoezi la kuwalipa fidia wananchi wa Kijiji cha Ngombo kilichopo ndani ya Pori la Akiba Kilombero Mkoani Morogoro linaendelea vizuri ambapo asilimia 93 ya wananchi wote tayari wamekwishalipwa fidia zao kwa ajili ya kupisha shughuli za uhifadhi katika Hifadhi hiyo na asilimia 7 ya wananchi waliosalia wanaendelea kushughulikiwa ili kukamilisha malipo yao.
Akizungumzia zoezi hilo Desemba 31, 2024 wilayani humo
Mhe. Sebastian amesema Serikali imetoa zaidi ya shilingi billioni 6.9 kulipa
wananchi 1,056 ili waweze kuhama kwa hiari kutoka maeneo ya Hifadhi huku akitoa
maelekezo kwa watendaji wa vijiji 32 wilayani Malinyi kuwapokea ili waweze
kuendelea na shughuli zao za kila siku.
"Kwanza si kweli kwamba wananchi wa Ngombo
hatujawaambia mahali pakwenda. Katika barua yangu ya tarehe 4 Disemba, 2024 niliyowaandikia
watendaji wa vijiji 32 vilivyo ndani ya wilaya ya Malinyi, nilitoa maelekezo ya
kuwapokea wananchi wa Kijiji cha Ngombo wanaopisha shughuli za uhifadhi katika
Pori la Akiba Kilombero, na ndivyo inavyofanyika na pia nilielekeza watendaji
hao wawataarifu wananchi wote kupitia mikutano ya hadhara," amesema.
"Na tangu wananchi wangu wa Ngombo walipoanza kuhama
kwenda katika maeneo yao waliyokwenda, sijapata lalamiko lolote kwa simu au kwa
mdomo kwamba wamezuiliwa kukaa mahali fulani na kwa taarifa nilizonazo baadhi
yao wamehamia sehemu mbalimbali ikiwemo Mikoa ya Lindi, Ruvuma, Pwani na
Halmashauri ya Mlimba. Kwahiyo mimi ninaamini mambo yanakwenda vizuri na ndivyo
ilivyo," amesisitiza Mhe. Sebastian.
Kuhusu wanafunzi waliokuwa wanasoma shule katika Kijiji
cha Ngombo, Mkuu huyo wa wilaya amesema amekwishatoa maelekezo kwa Afisa elimu
kuwapokea na kuwasajili katika shule
zilizopo kwenye vijiji vilivyo ndani ya wilaya hiyo bila masharti yoyote ili
waweze kusoma kwa uhuru.
Aidha, Mhe. Sebastian amesema wananchi wa Kijiji cha
Ngombo waliandaliwa mapema kwa kupewa elimu juu ya malipo ya fidia ili weweze
kuhama kutoka katika eneo la Hifadhi ya Kilombero tangu mwezi Agosti, 2024.
Hivyo, walikuwa na uelewa kuhusu zoezi hilo na amewataka kuepuka watu wenye nia
ovu ya kupotosha dhamira njema ya zoezi hilo.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Biro Bi.
Elizabeth Mnenuka amekiri kupokea zaidi ya wananchi 50 katika Kijiji cha Biro
na wengine zaidi ya 30 katika Kijiji cha Mbalinyi na kuongeza kuwa baadhi yao
tayari wameshapatiwa maeneo kwa ajili ya kuendeleza kwa kilimo na makazi.
Nao wananchi waliohamia Kijiji cha Biro kutoka Kijiji cha
Ngombo wameishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwalipa fidia zao Kwa wakati
ambazo zimewasaidia kuhama na kuanza maisha mapya katika vijiji jirani.
"Toka nitoke Kijiji cha Ngombo ambapo tuliondolewa
kisheria kwakweli sina changamoto yoyote kimaisha, niko vizuri naishi vizuri na
familia. Naishukuru Serikali, fidia nimepata kwahiyo mpaka hapa sina neno na
Serikali," amesema Daudi Deodatus Lyambu aliyekuwa mkazi wa Ngombo ambaye
sasa amehamia Kijiji cha Biro.
Ikumbukwe kuwa mnamo tarehe 17 Februari, 2023 Pori la
Akiba Kilombero lenye sehemu A na B lilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Namba
64 kufuatia kupandishwa hadhi kwa sehemu ya Pori Tengefu la Kilombero kuwa Pori
la Akiba.
Aidha, kufuatia kuanzishwa kwa Pori la Akiba Kilombero,
masharti na sheria zinazosimamia eneo hilo zilibadilika ambapo shughuli zote za
kibinadamu zimesitishwa isipokuwa zile zinazokubalika kwa mujibu wa sheria.
Lengo la Serikali likiwa ni kuimarisha usimamizi wa eneo hilo kwa kuhifadhi
vyanzo vya maji, misitu na wanyamapori ili kuongeza tija ikiwemo upatikanaji wa
maji kwa ajili ya uzalishaji wa umeme katika Bwawa la Mwl. Nyerere.
Na. Beatus Maganja- Malinyi
0 Maoni