WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiheshimisha Tanzania katika hamasa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kutokana na umuhimu wake kwenye afya ya binadamu na utunzaji wa mazingira.
Amesema kuwa kutokana na jitihada hizo, mashirika ya
kimataifa yameonesha nia ya kumuunga mkono ikiwemo kufanya mkutano mkubwa wa
nishati safi Afrika hapa nchini. “Watanzania tumuunge mkono Rais Dkt. Samia
katika kampeni hii na kuhakikisha tunaongoza kwenye matumizi ya nishati safi barani
Afrika.”
Amesema hayo leo (Jumanne, Desemba 31, 2024) wakati wa
Tamasha la Azimio la Kizimkazi ambalo lilienda sambamba na ugawaji wa majiko
1000 ya gesi kupitia kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia. Tukio hilo
limefanyika katika eneo la Kilimahewa Majumbakumi, Ruangwa mkoani Lindi.
“Tunapaswa kumuunga mkono kwasababu agenda imeanzishwa na
Rais wetu, dunia lazima iitambue Tanzania kama ambavyo imetambua na kuleta
mkutano mkubwa wa nishati safi hapa nchini, sisi tusiwe nyuma, tuwe mstari wa mbele.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Mamlaka za
Serikali za Mitaa kuibeba ajenda ya nishati safi ya kupikia na kuhamasisha
umuhimu wa matumizi ya nishati hiyo ikiwemo umeme, gesi na mkaa rafiki.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi
Zainab Telack amesema kuwa azimio la kizimkazi linakwenda kuwa mkombozi kwa
mwanamke kupata nishati safi ya kupikia.
Mmoja ya wanufaika wa mpango huo wa ugawaji wa mitungi ya
Gesi Hawa Mpinga mkazi wa Kata ya Nachingwea amesema awali walipata changamoto
za kiafya kutokana na matumizi na nishati chafu “Moshi wa kuni umetuharibu sana
macho.”
Katika tukio hilo Mheshimiwa Majaliwa amewaga mitungi ya
gesi 1000, ambayo 800 imetolewa na Shirika la Utangaji Tanzania kupitia Bongo
Fm na mitungi 200 imetolewa na Taifa gesi.
0 Maoni