Katika Mwamba Huu Nitalijenga Kanisa

 

Na. Mwandishi wetu, Ngorongoro 

Ilinenwa “KATIKA MWAMBA HUU NITALIJENGA KANISA”, ndivyo walivyofanya waumini  wa Parokia ya Mt. Petro Masanza  Kona mkoani Simiyu ambapo baada ya kulijenga kanisa kwa umoja wao waliamua kutembelea  hifadhi ya Ngorongoro kujionea uwezo wa mwenyezi Mungu katika uumbaji wa ulimwengu na vilivyomo.

Ziara hiyo imewashirikisha waumini 50 kutoka parokiani hapo wakiongozwa na  mapadri wanne na frateli mmoja ikiwa na lengo la kuwawezesha waumini kufanya utalii wa ndani na kujifunza juu ya urithi wa dunia ambao  upo ndani kasoko ya Ngorongoro.

Akiongoza ziara hiyo,Rev Fr. Furaha James ambaye ni Paroko wa Parokia ya Masanza  alisema kwamba ziara hiyo imekuwa na umuhimu mkubwa kwa kuwa wamepata fursa ya kujifunza historia, utamaduni, mazingira na vivutio vya asili vilivyopo nchini.

“Tumekuja hapa kwa ajili ya kujifunza na kuona kile ambacho Mungu ametujalia katika nchi yetu. Naamini kuwa waumini wetu waliotembelea hapa wameongeza uelewa na watakuwa mabalozi wa kutunza na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini kwetu” alisema Fr. Furaha .

Aidha kwa upande wa WAWATA, akiwemo Bi. Flora Nkolongo walieleza kufurahishwa na ziara hiyo, wakisema kuwa imewapa nafasi ya kujifunza na kuwaona wanyama mbalimbali kama Simba, Faru, Nyati, Tembo na wengine wengi ambao ni mara yao ya kwanza kuwaona kwa karibu.

Ziara hiyo ilihitimishwa  kwa kutembelea  makumbushi ya Urithi ambako walipata historia ya ardhi ya Ngorongoro, volkano, wanyamapori, maendeleo ya binadamu na tamaduni za jamii zinazozunguka eneo hilo ambao ni Wamasai, Wahadzabe, Wairaqw na Wadatoga na waumini hao kuhitimisha ziara yao kwa kuamini kuwa NGORONGORO NI NYUMBANI KWA KILA KIUMBE.




Chapisha Maoni

0 Maoni