Mbunge wa Musoma Vijijini Prof. Sopspeter Muhongo amewataka wakazi wa Mkoa wa Mara kujikita zaidi katika ufukaji wa samaki kwa njia ya vizimba pamoja na kilimo cha umwagiliaji katika mabonde ya Bugwema na Suguti.
Prof. Muhongo amesema wakazi wa Wilaya ya Musoma lazima
wapambane katika kupata mikopo mingi ya uwekezaji wa uvuvi wa vizimba, kwa kuwa
ndio uvuvi unaofanyika sehemu nyingi duniani na umeonekana kuleta tija.
“Uvuvi huu unafanyika dunia nzima hata bahari ya Hindi, bahari
ya Pacific, huko Mediteranean..samaki wameisha watu wanavua kwa vizimba, kwa
hiyo ndio uwekezaji namba moja,” amesema Prof. Muhongo na kuongeza,
“Na uwekezaji wa vizimba unapaswa kuendana na ujenzi wa
viwanda vya samaki, sio hivi ambavyo mnajenga, anatoka mwekezaji kutoka Kenya
anajenga, siku wakihama na viwanda vimehama.”
Amesema wanachokifanya sasa kule bungeni, ambapo yeye
yupo kwenye kamati wanajaribu kutafuta viwanda ili hata kule Musoma Vijijini
kuwe na viwanda vidogo vidogo vya kusindika samaki na vya kukausha dagaa.
Pia, Prof. Muhongo ameshauri waliomijini kwenda vijijini
kutafuta mashamba walime pamba na alizeti, kilimo ambacho kinapaswa kuendana na
ujenzi wa viwanda vya usindikaji ili kupata mafuta. Pamba pia itawawezesha
kupata kiwanda cha nguo.
0 Maoni