Wizara ya Afya Zanzibar imesema itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na Taasisi ya The Same Qualities Foundation kutoka Arusha, kwa lengo la kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Zanzibar, hususan matibabu ya watoto na watu wazima wenye tatizo la midomo wazi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor
Ahmed Mazrui, alipofanya ziara maalum katika kambi ya matibabu ya midomo wazi
inayoendelea kufanyika katika Hospitali ya Mkoa Lumumba. Kambi hiyo inaendeshwa
kwa ushirikiano kati ya madaktari bingwa kutoka taasisi hiyo ya Arusha na
wataalamu wa ndani kutoka Zanzibar.
“Matibabu yanayotolewa katika kambi hii ni bure kabisa na
dawa zipo za kutosha. Naomba niwasihi wazazi wenye watoto wenye matatizo haya
wawatoe majumbani, wawafikishe hospitalini ili wapatiwe huduma. Wakitibiwa
vizuri, wanarejea katika hali ya kawaida na kupata heshima yao katika jamii,”
alisema Waziri Mazrui.
Amesema kuwa, kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya, taasisi hiyo imekuwa ikileta mara
mbili kwa mwaka madaktari bingwa kutoka mataifa mbalimbali kutoa huduma hizo
bure kwa wananchi wa Unguja na Pemba.
“Tumeshuhudia wagonjwa waliopata huduma hizi katika awamu
zilizopita, wengi wao wanaendelea vizuri kiafya. Tunaamini hata safari hii
huduma zitatolewa kwa ufanisi mkubwa,” aliongeza Waziri Mazrui.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa waandaaji wa kambi hiyo,
huduma hizo za upasuaji na tiba za midomo wazi zimeanza kutolewa rasmi tangu
Jumatatu, Agosti 25, na zitahitimishwa Ijumaa, Agosti 29, ambapo jumla ya watu
25 wanatarajiwa kupatiwa matibabu.
The Same Qualities Foundation ni miongoni mwa taasisi zinazotoa mchango mkubwa katika sekta ya afya Tanzania Bara na Zanzibar, kwa kutoa huduma za kibingwa kwa watu wenye matatizo ya kinywa na uso, hasa midomo wazi, bila malipo.
0 Maoni