Dar es Salaam ya kijani CCM ikizindua kampeni za urais Kawe leo

 

Leo alasiri, macho na masikio ya Watanzania yataelekezwa viwanja vya Tanganyika Packers Kawe, jijini Dar es Salaam, ambako Chama cha Mapinduzi (CCM) kinatarajia kuzindua rasmi kampeni zake za urais kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025. 

Tangu jana eneo hilo limesheheni msisimko mkubwa wa kisiasa, huku maelfu ya wanachama na wafuasi wa CCM wakimiminika leo kwa wingi wakiwa wamevalia mavazi ya kijani na njano. Bila shaka, Dar es Salaam leo ni ya kijani, rangi ya matumaini kwa wanaccm na chama chao.

Mgombea wa urais kupitia CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuongoza uzinduzi huo pamoja na mgombea mwenza wake, Dkt. Emmanuel Nchimbi. Viongozi hao wawili wanasubiriwa kwa hamu kubwa ili kunadi sera na mwelekeo wa CCM kwa miaka mitano ijayo.

Hii itakuwa nafasi ya kwanza kwa Dkt. Nchimbi kujitambulisha rasmi kwa wananchi kama mgombea mwenza katika uchaguzi huu muhimu.

Kawe imegeuka kuwa kitovu cha siasa, huku vikundi vya burudani vikitoa viburudisho mbalimbali na kuhamasisha umati mkubwa wa wananchi na viongozi watakaohudhuriwa ufunguzi wa pazi la kampeni za urais za uchaguzi mkuu wa 2025.

Uzinduzi huu wa kampeni unatarajiwa kuashiria mwanzo wa safari ya CCM kuelekea kusaka ushindi. Macho na masikio yote sasa yapo Kawe, kusubiri kusikia sera na ahadi zitakazowasilishwa na viongozi hao wawili wanaoingia ulingoni kwa lengo la kuendelea kulitumikia taifa.

Chapisha Maoni

0 Maoni