Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi, Mtoto na Viashiria vya
Malaria Tanzania 2022, inaonesha kuwa vifo vitokanavyo na uzazi kwa wakina mama
wakati wa uzazi vimepungua kutoka vifo 530 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka
2015/16 hadi kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022.
Takwimu hizi zimetolewa leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati akizindua ripoti hiyo jijini Dar
es Salaam na kuongeza kuwa kwa sasa kiwango cha vifo vya uzazi kwa wakina mama nchini
kimepungua kwa asilimia 80.
“Kwangu binafsi kama kiongozi na kama mzazi naijua vyema
kazi inayofanyika kule ndani, na kutoka ukiwa hai basi ni baraka ya Mungu, sasa
nibaraka ya Mungu lakini ni Serikali kujipanga na vifaa ili matatizo
yanapotokea basi uweze kusaidiwa kwa haraka,” alisema Rais Dkt. Samia na
kuongea “Na kwa sababu nimesha pita huko kama mzazi na Mhe. Waziri wa Afya Ummy
Mwalimu alishapita huko kwahiyo tukasema tufunge kibwebwe tuifanye hii kazi.”
Amesema shabaha ya Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs yanaagiza
ifikapo 2030 vifo vitokanavyo na uzazi kwa kina mama wakati wa uzazi visizidi
70 kwa kila vizazi hai 100,000, “Sisi tupo 104, safari yetu mpaka 2030 tunaweza
kufikia hayo malengo”.
Rais Dkt. Samia amewataka madaktari na wakunga kutobweteka
na mafanikio hayo bali waende wakafanye kazi, kwani vifaa vipo wakafanye kazi
kwenda kuokoa uhai wa wakina mama wajawazito nchini.
Pia, ripoti hiyo imeonyesha kupungua kwa idadi ya vifo vya
watoto waliochini ya umri wa miaka 5, kutoka vifo 67 kwa kila vizazi hai 1,000
mwaka 2015/16 hadi kufikia vifo vya watoto 43 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka
2022.
“Kwa upande wa watoto wachanga hapa bado kunakazi ya kufanya
kwa sababu vimepungua kwa asilimia 1, na inawezekana kabisa hatukuwa na vifaa
vya kusaidia kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa,” alisema Dkt. Samia.
Rais Dkt. Samia amesimulia kwamba kunakipindi alienda
kumuangalia mjukuu wake aliyezaliwa njiti, alikuta hali ambayo ilimtoa machozi hospitalini
kwa mara nyingine tena, hakuna mashine vitoto vimepangwa kwenye mashine moja
vinalialia, wengine wamebebwa na mama zao.
“Nilipofika kwa mjukuu wangu nikamuaona amewekwa juu ya meza
anapigwa na taa kwa juu nikasema kwamba huyu mbona mumemweka hapa nikaambiwa anapata
joto hapa ndio anapata uhai wake,” alisema Dkt. Samia na kuongeza “Nikasema
kwamba hii hali hairidhishi leo namshukuru Mwenyezi Mungu ametusaidia tumegawa
vifaa 123 vya watoto njiti.”
Pamoja na mambo mengine ripoti hiyo imeonyesha kumekuwepo na
mafanikio ya kupungua kiwango cha mimba za utotoni kwa watoto wa kike wenye
umri wa kuanzia umri wa miaka 15 hadi 19, kutoka asilimia 27 mwaka 2015/16 hadi
asilimia 22 mwaka 2022.
Rais Samia ameitaja mikoa inayoongoza kwa kuwa na kiwango
kikubwa cha mimba za utotoni kuwa ni Songwe 45%, Ruvuma 37%, Katavi 34%, Mara 31%,
Rukwa 30%. Aidha, katika mikoa ya Dar es Salaam, Njombe na Ruvuma viwango vya
mimba za utotoni vimeongezeka.
0 Maoni