Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na
Uvuvi limefanikiwa kukamata jumla ya mifugo 400 ambayo ilikua inasafirishwa
kwenda nje ya nchi bila kufuata utaratibu.
Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi
wa Mifugo Nchini Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Simon Pasua leo Oktoba 28,
2023 amebainisha kuwa mifugo hiyo imekamatwa katika Wilaya ya Mkinga Mkoani
Tanga kupitia doria ambayo bado inaendelea na ilikua inatoroshwa kwenda nchi
jirani kwa njia za magendo.
Sambamba na hilo pia amesema kuwa katika kuhakikisha
wafugaji na wafanyabiashara wanafuata taratibu, kwa mwezi Oktoba mwaka huu
Jeshi hilo limefanikiwa kutoa elimu kwa wafugaji katika minada mbalimbali
nchini ambapo hadi kufikia Oktoba 28 jumla ya vipindi 149 vya elimu vimetolewa
kote nchini.
ACP Pasua amefafanua kuwa kupitia elimu ambayo wanaendelea
kuitoa imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya wizi wa mifugo sambamba
na migogoro ya wakulima na wafugaji.
Aidha, ametoa wito kwa wafugaji wote nchini kuacha mara moja
tabia ya kuhamisha mifugo kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine ama Nchi jirani
bila ya kufuata utaratibu wa kupata vibali toka serikalini, kwani Jeshi hilo
litachukua hatua za kisheria dhidi yao ikiwa ni pamoja na kukamata mifugo hiyo
na kuwafikisha mahakamani.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mnada wa Horohoro uliopo Mkoani
Tanga Bwana Edgar Ndombere pamoja na kulishukuru Jeshi hilo kwa doria ambayo
wanaendelea kuifanya, amesema changamoto wanayokutana nayo ni wafugaji wengi
kutokua na utayari wa kulipa kodi ambapo hupita sehemu ambazo sio rasmi.
Pia, ametoa wito kwa wafugaji hao kuwa wazalendo na kufuata
utaratibu uliowekwa kwa kuhakikisha wanapeleka mifugo yao katika maeneo ya minada
ili wapatiwe vibali kwa ajili ya kusafirisha mifugo yao.
Sehemu ya mifugo 400 iliyokamatwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambayo ilikua inasafirishwa kwenda nje ya nchi bila kufuata utaratibu.
Na. Mwandishi wetu Jeshi la Polisi
0 Maoni