Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imepewa maelekezo
ya kuhakikisha inawalea wafanyabiashara nchini kwa kurahisisha jinsi ya
kuifikia, kuwa mbunifu wa namna ya kuwahudumia na kuifanya taasisi kuwa ya Watanzania
ili kufikia malengo ya uanzishwaji wake.
Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara,
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji alipokuwa akifungua mkutano wa kwanza wa BRELA na wadau
wake jana kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Mhe. Dkt. Kijaji ameeleza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kukabidhi uchumi wa taifa
kwa sekta binafsi na amefungua mipaka yote, hivyo taasisi ya kwanza
inayoshughulikia sekta binafsi ni BRELA kwakuwa uchumi wa nchi unakua kupitia
ukuaji wa sekta ya viwanda na biashara nchini.
Ameongeza kwa kusema kuwa kuanzia mwaka 2019 hadi Juni, 2023
Serikali imeeendelea kutekeleza mpango wa kuboresha mazingira bora ya biashara
na kuondoa tozo na kodi mbalimbali zaidi
ya 374 zilizosumbua wafanyabiashara ambapo Serikali imefikia zaidi ya asilimia
75 ya dhamira yake.
“Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kupitia Sheria ya Fedha jumla
ya Sheria na Kanuni 13 na pia Sheria ya Fedha ya mwaka 2023 zimeweza kupunguza
na kufuta tozo, ada na faini 67 ikiwa na lengo la Serikali ya awamu ya sita la
kuhakikisha mazingira ya biashara kuwa bora zaidi,” ameeleza Mhe. Dkt.
Kijaji.
Mhe. Dkt Kijaji amesisitiza kuwa hakuna uchumi wa nchi
unaokua kama hakuna maendeleo katika sekta ya viwanda na ya biashara iliyo
imara, Serikali inahakikisha inaboresha mazingira ya ufanyaji biashara ndani na
nje ya Tanzania na taasisi za udhibiti hazitumii mamlaka zao kufungia biashara
yoyote lengo ni kuhakikisha kuwa sekta ya biashara inalea uchumi wa nchi.
Ameendelea kusema kuwa anatambua kuwa wafanyabiashara wapo
mbele zaidi, kwa kuwa dunia haiwezi kutusubiri hivyo kwa kasi hiyo Wizara ya
Viwanda na Biashara imeweka dhamira ya kuboresha Sera na Sheria ili zisomane na
mabadiliko ya uchumi.
“Tunaangalia uwekezano wa kutoa leseni zote za biashara
katika mfumo mmoja wa BRELA kuliko kuwa na mifumo mingi inayotoa huduma za
leseni za biashara hii itasaidia uratibu mzuri wa leseni za biashara na
Serikali kuwa na kanzi data moja ya taarifa za biashara, tunawaomba mtupe
ushirikiano katika hatua hii ili kuwahudumia kwa ufanisi mzuri," ameongeza
Mhe.Dkt Kijaji.
Mhe. Dkt. Kijaji amehitimisha kwa kuielekeza BRELA kutumia
mkutano huu kama sehemu ya kupokea maoni ya Watanzania, kuboresha na kutumia
vema maoni hayo na kila mwaka mkutano
mtakapokutana na wadau hawa muwe na mijadala yenye majibu ya utatuzi wa
changamoto zao
Nae Mbunge wa Kahama Mjini, Mhe. Jumanne Kishimba akiongea
kwa niaba ya wafanyabiashara walioshiriki mkutano huo amesema wafanyabiashara
wengi hukimbilia huduma za BRELA ili kupata huduma za mikopo kutoka taasisi za
fedha na kupata zabuni ila wengi hawaelewi tafsiri za kisheria za kampuni,
hivyo ameishauri kuweza kuzitafsiri kwa lugha nyepesi ili kuepusha migogoro
mbalimbali.
Awali katika hotuba yake, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA,
Godfrey Nyaisa ameeleza kuwa anatambua kuna sheria nyingi ambazo zimepitwa na
wakati na ipo kwenye hatua za maboresho ya sheria mbalimbali kama vile
Maboresho ya Sheria ya Viwanda ya mwaka 1967, Maboresho ya Sheria ya Hataza ya
Mwaka 1987, Maboresho ya Sheria ya Miliki Bunifu ya Mwaka 1986 na Maboresho ya
Sheria ya Kampuni ya Mwaka 2002 ili ziendane na mabadiliko ya Kiteknolojia na
ukuaji wa sekta ya biashara.
Akihitimisha Mkutano huo wa Wadau, Mwenyekiti wa Bodi ya
Ushauri ya BRELA, Prof. Neema Mori, amehitimisha kwa kuwaahidi wadau kuwa
wamepokea maoni yote ya wadau na kuwahakikishia kuwa Bodi itasimamia Taasisi
ili kuleta urahisi wa matumizi ya mifumo kuwa kidigitali na kidigiti na
itaendelea kusimamia michakato ya kuwepo kwa Sera na maboresho ya sheria mbalimbali.
0 Maoni