Kauli ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu
Nchemba, kwamba kiasi cha Dola za Marekani milioni mbili (sawa na takribani
Shilingi Bilioni 4.5) zimetolewa kwa ajili ya kuchochea chokochoko na vurugu
nchini, limezua mjadala mkali mtandaoni.
Watumiaji wa mitandao ya kijamii
wamejikita katika kuchambua chanzo cha vurugu, maslahi ya mataifa ya kigeni, na
umuhimu wa busara katika kushughulikia masuala ya kitaifa.
Waziri Mkuu alisema kuwa
wachochezi wamelenga kuharibu uchumi wa nchi na kurudisha nyuma maendeleo, huku
lengo kuu likiwa ni kunyakua rasilimali adimu za Tanzania kama vile madini ya
Uranium na maendeleo ya miradi ya gesi asilia.
Baada ya ufichuzi huo, maoni
yamegawanyika kati ya wale wanaosisitiza umuhimu wa kufahamu maslahi ya Taifa
na wale wanaotilia mkazo umakini wa vijana kujitambua.
Mchangiaji Oliver Kibua
alikaribisha ufichuzi wa Serikali, akisisitiza umuhimu wa wananchi kujua chanzo
na sababu ya vurugu hizo:"Afadhali kama inaweza kuwaambia wananchi sababu
na chanzo cha yote wajue kipindi watu wanatumika na kuhadaika kuwa wapiganie
haki kumbe wenzao wana wanachokitaka, na vurugu ikiwepo waumiao ni wananchi
waliopo nchini na sio nje ya nchi."
Kibua pia alisisitiza kuwa
wananchi wanapaswa kufahamu kuwa hakuna taifa linaloingilia kati masuala ya
nchi nyingine bila maslahi yao binafsi. Alihimiza, "Hao wanaojitambua
waamke maana wanajitambua wao hawatambui ukweli wa mambo... think before you
act."
Mchangiaji mwingine alitumia
nafasi hiyo kukosoa matumizi ya lugha ya matusi na mihemko katika mijadala ya
kitaifa, hasa kwa wale waliowahi kushika nyadhifa za uongozi.
"...Nikuona watu waliowahi
kuwa madarakani mahali fulani wakakosana na waliowaweka madarakani wanavyokuwa
hawajui kutumia lugha ya ushawishi na badala yake wanatukana... Si suala tu la
kuamsha hisia bali ni suala la kusoma, kutafakari na kuona kweli katika muda
sahihi na mazingira sahihi." alisema mmoja wa wachangiaji hao.
Mchangiaji huyo alitumia fumbo la
kijadi kuhusu njiwa waliokosa ushauri na kufa ufukweni, akisisitiza kuwa nguvu
(mihemko) bila maarifa (busara na ushauri) haisaidii. Alihimiza Watanzania
kuchanganya maarifa ya kimagharibi na hekima za zamani ili kupata majibu
sahihi.
Hata hivyo Rafael Valency Kwembe
alionyesha imani kwa vijana wa Afrika, akisema:"Uzuri waafrika wa sasa
tunajitambua sana, nyie pigeni ngonjera ila ukweli tunaujua na tunaufanyia
kazi. Tunajua nani anazingua na nani yupo sahihi."
Mchangiaji mwingine aliunga mkono
msimamo wa Serikali kwamba vurugu hizo zinaletwa na wanaharakati wanaolipwa na
kuwahimiza Watanzania kuamka na kuchukua tahadhari, akisisitiza: "Ajira na
uondoaji wa umaskini utapatikana tu nchi ikiwa na amani."
Kauli ya Waziri Mkuu inahimiza
Watanzania kujiuliza maswali kuhusu maslahi na ajenda ya watu wanaotoa malipo
hayo. Alionya kuwa mbinu hizi zimetumika katika nchi zingine barani Afrika,
ambapo chokochoko huanzishwa ili kuruhusu uvurugaji na uchukuaji wa rasilimali,
kabla ya wachochezi kuondoka baada ya rasilimali kuisha.

0 Maoni