Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani
Moshi Mkoani Kilimanjaro, wameishukuru Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini
(TARURA) kupitia mradi wa RISE kwa kuanza kukarabati barabara ya Mabogini–Kahe
ambayo kwa miaka mingi ilikuwa katika hali mbaya na imekuwa chanzo cha adha
kubwa kwa wakazi wa eneo hilo.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 31 imekuwa ni
changamoto kwa wakazi wa Mabogini na vijiji vya jirani, hasa nyakati za mvua
ambapo ilikuwa haipitiki kutokana na mashimo, maporomoko ya maji na kukosekana
kwa mifereji ya kupitisha maji.
Wakizungumza, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamesema
hatua ya Serikali kuanza ukarabati wa sehemu ya barabara hiyo kwa kiwango cha
changarawe imeanza kuleta nafuu kubwa katika usafirishaji wa mazao na shughuli
nyingine za kijamii na kiuchumi.
Bw. Hasani Halifa mkazi wa Mabogini amesema kuwa barabara
hiyo licha ya kuwa bado ina changamoto katika baadhi ya maeneo, lakini imeleta
unafuu wa takribani asilimia 60 kwa wakulima na wasafirishaji.
“Kabla ya ukarabati huu, tulikuwa tunasafirisha mazao kwa
gharama kubwa nauli ilikuwa kati ya Sh. 7,000 hadi Sh. 10,000 kwa mzigo mmoja
kutoka shamba hadi sokoni lakini sasa tunatumia Sh. 1,000 hadi Sh. 2,000 tu”,
amesema.
Kwa upande wake, mkulima na kiongozi wa skimu ya umwagiliaji
ya Kaloleni, Bw. Hamis Mohamed amesema
kuwa awali walikuwa wakipata hasara kubwa kutokana na kushuka kwa bei ya
mazao sokoni kwa sababu wanunuzi walishindwa kufika mashambani kutokana na hali
mbaya ya barabara.
“Mazao yalikuwa yakiozea shambani, tulishindwa kuyatoa kwa
wakati, wakati mwingine hata kupatikana kwa magari ilikuwa shida. Mradi huu wa
barabara kwetu wakulima ni wa thamani kubwa”, amesema.
Hata hivyo, wakazi hao wameiomba Serikali kuendeleza
ukarabati huo kwa kuweka lami nyepesi
ili barabara hiyo iweze kudumu zaidi na kuhimili hali ya hewa ya eneo
hilo, hususan mvua kubwa na jua kali linalosababisha vumbi.
Naye, Mwenyekiti wa Kkitongoji cha Mabogini Juu, Bw. Zuberi
Bakari amesema hali ya barabara hiyo ilikuwa mbaya kiasi kwamba watoto
walishindwa kwenda shule msimu wa mvua huku wajawazito wakikosa huduma za afya
kwa wakati, jambo lililosababisha hata baadhi yao kupoteza maisha.
“Tulikuwa tunapitia shida kubwa nyakati za mavuno, mazao
mengi yalikuwa yanaharibika mashambani. Hali ya barabara ilikuwa ya kuumiza
moyo. Tunaiomba serikali ituwekee hata lami ya kiwango cha kati”, amesema.
Naye, Meneja wa TARURA wilaya ya Moshi, Mhandisi Godfrey
Mbema ameeleza kuwa barabara ya Mabogini–Kahe ina urefu wa kilomita 31, ambapo
kwa sasa kiasi cha kilomita 1.2 kimeanza kukarabatiwa kwa kiwango cha
changarawe chenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 800, ikiwa ni sehemu ya
mpango wa muda mfupi wa kuboresha miundombinu ya vijijini.
Serikali kupitia TARURA imeendelea kutekeleza miradi
mbalimbali ya barabara katika maeneo ya vijijini kwa lengo la kuinua uchumi wa
wananchi kupitia miundombinu bora inayowezesha biashara, usafirishaji na
upatikanaji wa huduma za kijamii.


0 Maoni