Uandishi wa habari za sayansi kwa umakini na umahiri
ni nyenzo muhimu ili kufikisha ujumbe sahihi kwa jamii, kusaidia kukuza
maendeleo ya tafiti na vumbuzi mbalimbali.
Bara la Afrika bado lina uhitaji mkubwa wa waandishi
wa habari ambao wamejikita na wapo na umahiri katika kuwasilisha masuala ya
sayansi kwa lugha rahisi zinazoeleweka kwa jamii.
“Kazi yoyote ile tunayoifanya [katika] sayansi ina
maana tu pale inapofahamika vizuri kwa watu na jamii nzima,”.
Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Afrika
Kusini Profesa Blade Nzimande amesema hayo alipokuwa akifungua rasmi Mkutano wa
13 wa Waandishi wa Habari za Sayansi Duniani.
Mkutano huo WCSJ2025 unafanyika Pretoria Afrika Kusini
kuanzia Disemba 1-5, 2025 ukiwa na kauli mbiu isemayo 'Uandishi wa sayansi,
unaojenga uelewa na uthabiti wa sayansi na haki za kijamii'.
“Nilipoombwa kuja kufungua mkutano huu nilikubali mara
moja kwa sababu ya umuhimu wa nafasi ya waandishi wa habari za sayansi katika
kukuza sayansi,” amesema.
Ameongeza “Kwa hiyo waandishi wa habari ni daraja
muhimu sana [lakini] hatusemi daraja lisilo na ukosoaji, hapana bali daraja muhimu la kuielimisha jamii
kuhusu sayansi.
“Kama bara, tunahitaji waandishi wa habari za sayansi
wengi kwa sababu bado tunalo jukumu la kuendeleza sayansi, teknolojia na
ubunifu barani Afrika.
“Na mawasiliano ni sehemu muhimu ya hilo. Kwa mfano,
tunayo mkakati wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa Afrika [STISA 2034].
“.., ambao unalenga kukuza sayansi, utafiti na
maendeleo barani Afrika jambo muhimu sana. Kwa hiyo tunathamini kazi
mnayofanya, na ni muhimu sana,” amesema.
Amesema waandishi wa habari wanapaswa kusaidia Bara la
Afrika kupambana na dhana potofu na ubaguzi katika namna sayansi
inavyowasilishwa.
“Lazima tuwahusishe pia makundi yaliyotengwa wanawake,
watu waliodhulumiwa au waliokuwa na historia ya ukandamizaji ili nao wawe
sehemu ya mawasiliano ya sayansi.
“Moja ya hatari kubwa inayoweza kuua umuhimu wa
sayansi ni kuifanya kuwa mradi wa viongozi au watu wachache.
“Sayansi haipaswi kuwa mradi wa tabaka la juu; lazima
iwe mradi unaoeleweka na watu wote. Tunawahimiza kuhakikisha mnazingatia hilo
kama waandishi wa sayansi,” amesema.
Prof. Nzimande ameongeza “Waandishi wa habari mnapaswa
kukabiliana na changamoto ya taarifa za uongo [fake news].
“Hili ni mojawapo ya mambo hatari sana katika
mawasiliano leo, mitandao ya kijamii ina mazuri na mabaya.
“Ni mazuri kwa kuwa kila mtu anaweza kupata
taarifa siku hizi karibu kila mtu
anasema,” amesema na kuongeza
“Mimi ni mtengeneza maudhui.” Lakini pia mitandao ya
kijamii inaweza kusambaza taarifa za uongo haraka sana, jambo ambalo ni hatari.
“Katika sayansi, tunapaswa kupambana na taarifa za
uongo, si tu katika jamii kwa ujumla, bali katika sayansi haswa kwa sababu
inaweza kusababisha madhara makubwa.
Amesisitiza “Je, mnakumbuka wakati wa COVID jinsi
taarifa za uongo zilivyosambaa?
“Leo kuna watu katika nchi kubwa wanaodai kwamba
chanjo husababisha autism jambo la uongo
kabisa.
“Lakini likirudiwa na watu wenye mamlaka, linakuwa
hatari zaidi. Hii ina maana kwamba lazima muwe jasiri kama waandishi.
“Mnapaswa kuwa jasiri na msiogope kuuliza maswali
makubwa na muhimu,” amesema.
Teknolojia ya Akili Unde [AI] katika sekta ya habari
pia si suala la kuliacha nyuma, amesisitiza,
“Tunahitaji kuingiza teknolojia mpya kama akili bandia
katika kazi yenu, ili kuimarisha weledi na uwazi katika taaluma yenu.
“Tunapaswa pia kushughulikia tofauti katika namna
sayansi inavyoripotiwa. Bara letu bado linatengwa katika mambo mengi.
“Mnachukua jukumu la kuhakikisha masuala ya sayansi
yanawafikia Waafrika si hivyo tu.
“Bali pia kuhakikisha ubunifu, uvumbuzi na miradi ya
sayansi kutoka Afrika inatambulika ndani
na nje ya bara,” amesema Prof Nzimande.
Diplomasia ya sayansi pia waandishi wa habari wanalo
jukumu la kusaidia kuikuza ndani ya Bara la Afrika.
“Sayansi haina mipaka, na kwa sababu hiyo ina uwezo
mkubwa wa kujenga mahusiano ya kidiplomasia baina ya nchi na mabara.
“Kama Afrika Kusini, tunaamini sana katika sayansi
huria kwamba sayansi inapaswa kufikika zaidi na iwe wazi.
“Lakini lazima niseme kwamba waandishi wa habari za
sayansi ni sehemu muhimu sana mjue au msijue katika kazi tunazofanya katika
sekta ya sayansi.
“Bila ninyi, hatuwezi kuwafikia wale tunaopaswa
kuwafikia,” amesema Prof Nzimande.

0 Maoni