WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Watanzania
wanataka kuiona nchi yao ikifikisha lengo la uchumi wa kati wa dola za Marekani
trilioni moja ifikapo mwaka 2050 na watakaofanikisha jambo hilo ni sekta
binafsi ikiwemo wenye wabunifu kutoka kwenye kampuni changa.
“Mtakumbuka kuwa Julai, mwaka huu Mheshimiwa Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan alizindua DIRA 2050. Dira hii si ya Serikali peke yake bali
ni kielelezo cha matarajio ya Watanzania ambao wanataka nchi yao ifikie uchumi
wa kati wa dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050. Injini ya
kuendesha nchi kuelekea maono haya ni sekta binafsi zikiwemo kampuni changa
zinazoanzishwa,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Desemba
03, 2025) wakati akifunga maadhimisho ya Wiki ya Kampuni Changa za Teknolojia
(start-ups) kwenye ukumbi wa PSSSF, Makumbusho, jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa akimwakilisha Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan, amesema kazi ya kufikisha lengo siyo ndogo na inahitaji
mabadiliko ya kiutendaji na kimtazamo. “Hatuwezi kufikia uchumi wa dola
trilioni moja kwa kuendelea kuuza bidhaa ghafi au kufanya mabadiliko kidogo tu.
Inatutaka tuwe na mbinu bunifu zenye tija: tuwe na njia mipya za kufanya mambo,
tuanzishe makampuni mapya, tuwe na bidhaa mpya na teknolojia mpya zinazoweza
kukua mara 10 badala ya asilimia 10.”
“Inahitaji tuje na ubunifu wa Kitanzania utakaovutia
mataifa na kuzalisha masoko ya nje. Inawezekana kabisa, twendeni tuunganishe
nguvu,” amesisitiza.
Amesema vijana waliochukua hatua ya kuanzisha kampuni
changa wao ndiyo wenye hatma ya Tanzania na kwambo njia hiyo ndiyo sahihi ya
kutenda kwa njia mbadala. “Nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na changamoto ya
vijana kutojiamini. Lakini wapo wengi ambao wametoa ajira kwa vijana wenzao. Na
hii ndiyo njia sahihi ya kufanya mambo kwa njia mbadala kama ambavyo wenzeyu
wamefanya.”
Amewataka Watanzania waiheshimu sekta binafsi kama
wanavyoiheshimu sekta ya umma kwa kuanza kubadilisha mtazamo wao ikiwemo
nidhamu ya utendaji kazi. “Kwa mazingira ya sasa, hakuna nchi imeweza kujenga
uchumi mkubwa bila kuishirikisha sekta binafsi. Hiki mnachokifanya ndiyo injini
ya kukuza uchumi,” amesema.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na
washiriki wa maadhimisho hayo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Anjela
Kairuki alisema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kampuni changa
ambapo hadi sasa kampuni changa za Kitanzania zinakadiriwa kufikia 1,041 na
kuzalisha ajira zaidi ya 140,000.
Alisema hadi kufikia mwaka 2024, kampuni hizo zilikuwa
zimeingiza mapato ya dola za marekani milioni 96.4 na kwamba hadi kufikia sasa
zimekwishafikisha mapato ya dola za Marekani milioni 300.
Alisema kampuni nyingi zinazochipukia zimejielekeza
kwenye matumizi ya teknolojia za huduma za kifedha, kilimo, afya, elimu na
kwamba bado wanatarajia kuwa na bunifu nyingi za kidijitali.


0 Maoni