Jeshi la Polisi
nchini Tanzania limetoa wito kwa wananchi wanaowafahamu watu wanaoshiriki
katika makundi ya mtandaoni yanayoeneza taarifa za uzushi, uchochezi, na uongo
zenye lengo la kuhamasisha vurugu na vitendo ambavyo ni kinyume na sheria,
watoe taarifa haraka iwezekanavyo kwao.
Kwa mujibu wa
taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu ya Polisi,
Dodoma, Makosa ya Kimtandaoni (Cybercrimes) na yale yanayohusisha uvunjifu wa
sheria hayatasamehewa. Jeshi hilo limetoa namba za simu za kutoa taarifa kwa
siri, ambazo ni: 0699 99 88 99, 0787 66 83 06, au kupitia kiunganishi cha
mtandaoni: https://taarifa.tpf.go.tz.
Wito huu umetolewa
huku Jeshi la Polisi likijulisha umma kwamba, hadi jioni ya leo tarehe
10/12/2025, hali ya nchi kiasalama, hasa katika shughuli za kiuchumi na
kijamii, inaendelea katika mazingira ya amani na utulivu.
Taarifa ya Polisi
inasisitiza kwamba wito huo umelenga kuhakikisha usalama unadumishwa kwa kupata
taarifa za mapema kuhusu watu wanaojaribu kuharibu amani hiyo kupitia mitandao.
Wananchi wameombwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha
utulivu na amani ya nchi inalindwa kwa manufaa ya wote.

0 Maoni